Korea Kaskazini yasajili kifo cha kwanza cha Covid - 19

Muhtasari

• Watu sita walifariki baada ya kuugua homa huku mmoja akipatikana na virusi vya Omicron, vyombo vya habari vya serikali viliripoti Ijumaa.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un alionekana akiwa amevaa barakoa kwenye runinga kwa mara ya kwanza siku ya Alhamisi kuagiza watu wafunge watu kufuli nchini kote. Picha: GETTY IMAGES
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un alionekana akiwa amevaa barakoa kwenye runinga kwa mara ya kwanza siku ya Alhamisi kuagiza watu wafunge watu kufuli nchini kote. Picha: GETTY IMAGES

Korea Kaskazini imethibitisha kifo chake cha kwanza kutokana  na virusi vya Covid-19, huku vyombo vya habari vya serikali vikiongeza kuwa makumi ya maelfu zaidi wanaugua dalili za homa hiyo.

Watu sita walifariki baada ya kuugua homa huku mmoja akipatikana na virusi vya Omicron, vyombo vya habari vya serikali viliripoti Ijumaa.

Ilisema watu 187,000 walio na homa walikuwa "wakitengwa na kutibiwa".

Wakati wataalam wanaamini kuwa virusi hivyo vimekuwepo nchini kwa muda mrefu, viongozi walitangaza visa vya kwanza Alhamisi.

Walisema kumekuwa na mkurupuko wa aina ya Corona iitwayo Omicron katika mji mkuu, Pyongyang, na kutangaza hatua za kutoingi au kutoka mjini humo. Hawakutoa nambari sahihi za visa vya maambukizi.

Lakini katika sasisho siku ya Ijumaa, shirika rasmi la habari la KCNA liliripoti kwamba mlipuko huo ulienea zaidi ya mji mkuu.

"Homa ambayo sababu yake haikuweza kutambuliwa ilienea kote nchini kutoka mwishoni mwa Aprili," ilisema.

Takriban watu 350,000 walikuwa wameonyesha dalili za homa hiyo, iliongeza, bila kutaja ni wangapi wamepima virusi vya Covid.

Idadi ya wakazi wake milioni 25 wako hatarini kutokana na ukosefu wa mpango wa chanjo na huduma duni za afya, wataalam wanasema.

Korea Kaskazini ilikataa ofa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ya kusambaza mamilioni ya chanjo za AstraZeneca zilizotengenezwa China mwaka jana. Badala yake, ilidai ilikuwa imedhibiti Covid kwa kufunga mipaka yake mapema Januari 2020.

Nchi hiyo inapakana na Korea Kusini na Uchina, ambazo zote zimepambana na milipuko ya Corona.

Siku ya Ijumaa, KCNA iliripoti kwamba kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un alikuwa ametembelea kituo cha afya na "kujifunza kuhusu kuenea kwa Covid-19 kote nchini".

Ilielezea hali hiyo kama "tatizo la haraka la afya ya umma".

Katika mkutano ulioangazia sheria mpya za Covid mnamo Alhamisi, Bw Kim alionekana amevaa barakoa kwenye runinga kwa kile kinachoaminika kuwa mara ya kwanza.

Kuna hofu kwamba mlipuko mkubwa unaweza kuifanya iwe vigumu zaidi kwa vifaa muhimu kuingia nchini, na kusababisha uhaba wa chakula na uchumi kudorora.

Korea Kusini imesema ilitoa msaada wa kibinadamu baada ya tangazo hilo la Alhamisi, lakini Pyongyang bado haijajibu.

Licha ya madai ya hapo awali ya Korea Kaskazini kwamba ilikuwa na "mafanikio mema" katika kuzuia Covid, kumekuwa na ishara wakati wote wa janga la uwepo wake nchini.