Somalia yapata rais mpya

Muhtasari

•Hassan Sheikh Mohamud alimshinda rais wa sasa, Mohamed Abudallahi Farmajo, ambaye amekuwa ofisini tangu 2017.

•Bw Mohamud aliapishwa muda mfupi baada ya matokeo ya mwisho kutangazwa, jambo lililosababisha wafuasi katika mji mkuu kushangilia na kufyatua bunduki hewan

Hassan Sheikh Mohamud atahudumu kama rais wa Somalia kwa miaka minne, akirejea wadhifa wake aliokuwa nao kati ya 2012 na 2017
Hassan Sheikh Mohamud atahudumu kama rais wa Somalia kwa miaka minne, akirejea wadhifa wake aliokuwa nao kati ya 2012 na 2017
Image: REUTERS

Kiongozi wa zamani wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amechaguliwa kuwa rais baada ya kura ya mwisho ambayo ilikuwa wazi kwa wabunge wa nchi hiyo pekee.

Alimshinda rais wa sasa, Mohamed Abudallahi Farmajo, ambaye amekuwa ofisini tangu 2017.

Kura hiyo ilihusisha tu Wabunge 328 wa Somalia kutokana na wasiwasi wa usalama wa kufanyika kwa uchaguzi mpana zaidi, na mmoja wao hakupiga kura.

Bw Mohamud alipata kura 214 na kumshinda Bw Farmajo aliyepata kura 110.

Wabunge watatu wanaripotiwa kuharibu kura zao.

Mazingira yasiyo ya kawaida yanaangazia masuala ya usalama wa Somalia pamoja na ukosefu wa uwajibikaji wa kidemokrasia.

Matokeo hayo yanaashiria kurejea kwa Hassan Sheikh Mohamud, ambaye alihudumu kama rais wa Somalia kati ya 2012 na 2017 kabla ya kushindwa na Bw Farmajo.

 

Uchaguzi huo - ambao ulikuwa na upinzani mkali hadi kwenda kwa raundi ya tatu - ulicheleweshwa kwa karibu miezi 15 kutokana na vita na masuala ya usalama.

Bw Mohamud aliapishwa muda mfupi baada ya matokeo ya mwisho kutangazwa, jambo lililosababisha wafuasi katika mji mkuu kushangilia na kufyatua bunduki hewani. Atahudumu kwa miaka minne ijayo.

Katika upigaji kura siku ya Jumapili, mamia ya wabunge walipiga kura zao kwenye jumba la ndege lenye ngome katika mji mkuu Mogadishu.

Milipuko ilisikika karibu na wakati upigaji kura ukiendelea, lakini polisi walisema hakuna majeruhi walioripotiwa.

Akiwa rais ajaye, Bw Mohamud atalazimika kukabiliana na athari za ukame unaoendelea ambapo Umoja wa Mataifa unasema Wasomali milioni 3.5 wako katika hatari ya kukumbwa na njaa kali.

Lakini kazi kubwa anayokabiliana nayo ni kunyakua udhibiti wa sehemu kubwa ya Somalia kutoka kwa al-Shabab. Kundi la wapiganaji wa Kiislamu lenye mafungamano na al-Qaeda linaendelea kutawala sehemu kubwa za nchi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara mjini Mogadishu na kwingineko.

Nchi hiyo pia inaathiriwa na mfumuko wa bei wa vyakula na mafuta uliosababishwa na vita nchini Ukraine.

Serikali inaungwa mkono katika mapambano yake dhidi ya al-Shabab na Umoja wa Afrika, kwa umbo la wanajeshi 18,000 na Umoja wa Mataifa.

Kukosekana kwa utulivu ni sababu mojawapo iliyoifanya Somalia kushindwa kufanya uchaguzi wa moja kwa moja. Somalia haijawahi kuwa na uchaguzi wa kidemokrasia wa mtu mmoja kwa kura moja tangu 1969.

Kura hiyo ilifuatiwa na mapinduzi, udikteta na mzozo uliohusisha wanamgambo wa koo na Waislam wenye msimamo mkali.

Hii ni mara ya tatu tu kwa uchaguzi usio wa moja kwa moja wa rais kufanyika nchini Somalia kwenyewe. Zilizotangulia zilifanyika katika nchi jirani za Kenya na Djibouti.