Wanajeshi walinda amani wa Tanzania wajeruhiwa katika mapigano na M23 DRC

Muhtasari

• Kundi la M23 linasema kuwa majeshi ya FARDC na MONUSCO ndio waliokuwa wa kwanza kufanya mashambulizi dhidi yao katika ngome yao iliyopo katika eneo la Jomba Jumatatu.

Wanajeshi wa MONUSCO walipambana na M23 mwezi uliopita
Wanajeshi wa MONUSCO walipambana na M23 mwezi uliopita
Image: AFP

Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, FARDC, limetangaza kuwa wanajeshi watatu wa Tanzania wanaohudumu katika kikosi cha walinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO wamejeruhiwa wakati wapiganaji wa M23 waliposhambulia ngome yao iliyopo Rutshuru.

MONUSCO imethibitisha kuwa wanajeshi wake watatu wamejeruhiwa na kupelekwa kutibiwa katika hospitali ya mjini Goma uliopo mashariki. Katika tangazo hilo jeshi la serikali ya Congo limesema mmoja wa wanajeshi hao amejeruhiwa vibaya.

Kundi la M23 linasema kuwa majeshi ya FARDC na MONUSCO ndio waliokuwa wa kwanza kufanya mashambulizi dhidi yao katika ngome yao iliyopo katika eneo la Jomba Jumatatu.

Hii inakuja wakati mapigano yakiendelea kwa siku ya nne mfulurizo kati ya pande hizo yaliyoibuka baada ya mapigano hayo kusitishwa kwa muda wa wiki mmoja- mapigano yanayoendelea katika eneo la Rutshuru katika eneo la Kivu ya Kaskazini.

MONUSCO ilitangaza kuwa ipo katika mapigano ikilisaidia jeshi la Congo, FARDC linalopigana na wapiganaji wa M23.

Tanzania ina wanajeshi zaidi ya 800 katika kikosi cha MONUSCO kinachohudumu Mashariki mwa DRC.

Katika taarifa yake iliyotolewa Jumatano usiku, jeshi la DRC, FARDC linaishutumu Rwanda kutuma kikosi chake maalum cha wanajeshi 500 kuwasaidia wapiganaji wa M23, likisema kuwa walikuja wakiwa wamevalia mavazi yenye rangi ya kijani kibichi na nyeusi.

Serikali ya Rwanda kwa upande wake imekuwa ikikana mara kwa mara kuwa inawasaidia M23, ikisisitiza kuwa tatizo lao liko ndani ya nchi yao wenyewe ya DRC.

Kikundi cha M23 Jumatano pia kilitoa tangazo kikiishutumu serikali kwa ‘’kuchagua njia ya vita’’, kwa vikosi vyake kushirikiana na wanajeshi wa MONUSCO na wapiganaji wa kundi linaloshutumiwa na Rwanda kufanya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 la FDLR kuwashambulia.

Tangazo hil la M23 linasema: “Kuchagua vita kwa serikali ya Congo badala ya kuchagua mazungumzo ya amani, ni tatizo katika kurejesha amani katika mashariki mwa DRC”.

Wakati huo huo, jeshi la DRC- FARDC limetangaza kuwa maazimio ya kikao cha wakuu wa majeshi kilichofanyika Goma ya kubuni kikosi maalumu cha kupigana na makundi ya wanamgambo mashariki mwa Congo, yatawasilishwa mbele ya kikao cha wataalamu wa masuala ya kijeshi na wakuu wa majeshi kitakayofanyika kati ya tarehe 15 na 19 mwezi huu mjini Nairobi Kenya, kabla ya kuidhinishwa na marais wa Kanda.