Tanzania yatakiwa kuondoa maafisa wa polisi Ngorongoro

Muhtasari

•UN imeitaka Tanzania kuondoa maafisa wake wa usalama Loliondo ili kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu.

•Serikali ya Tanzania ilipuuzilia mbali ripoti  kwamba baadhi ya raia wake walikimbia nje ya nchi kutafuta matibabu.

Image: BBC

Umoja wa mataifa (UN) umeitaka Tanzania kuondoa maafisa wake wa usalama Loliondo ili kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji unaodaiwa kufanyika katika eneo hilo ili kuruhusu waandishi wa habari, wanasheria, waangalizi wa haki za binadamu na asasi za kiraia kuingia Loliondo, kuzungumza na Wamasai walioathirika na kuripoti hali hiyo bila vitisho.

Kupitia taarifa ,Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wenyeji ama watu wa asili limeeleza kusikitishwa kwake na juhudi zinazoendelea za kuwaondoa zaidi ya Wamasai 70,000 wa tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro, Tanzania kutoka eneo la kilomita za mraba 1,500, ambazo ni ardhi ya vijiji iliyosajiliwa kisheria.

Jukwaa hilo limesema kwamba mnamo Juni 8, lilipata taarifa kuwa polisi wa Tanzania kwa kutumia nguvu, ikiwa ni pamoja na kutumia silaha kiholela, waliwaondoa kwa nguvu Wamasai katika ardhi zao na kusababisha makumi ya watu kujeruhiwa huku baadhi ya watu wakikimbilia msituni. Pia iliripotiwa matukio mbalimbali ya kukamatwa kwa viongozi wa jamii hiyo, wakiwemo Madiwani wa Vijiji na Wenyeviti. Umoja wa mataifa unataja vitendo hivi kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu na za Wamasai wa Loliondo.

Tanzania imesema nini hadi sasa?

Serikali ya Tanzania tayari imekwisha jibu shutuma mbali mbali ambazo zimekuwa zikitolewa huku wakitaka raia na wanaharakati kuto changanya uondokaji wa watu kwa hiari katika hifadhi ya ngorongoro na uwekwaji wa mipaka katika eneo la Loliondo ambapo ndipo mvutano unapodaiwa kutokea.

Msemaji wa serikali Gerson Msigwa akizungumza na BBC amesema serikali haijaenda kuwaondoa Wamasai Loliondo au Ngorongoro ila wananchi wamepewa fursa ya kujiondoa kwa uhiari ili kupisha utunzaji wa mazngira .

'Hakuna askari,serikali ama kiongozi serikali aliyetumwa kumuondoa mwananchi ama Masai kwenye makazi yake'

Bw.Msigwa amesema katika eneo la Ngorongoro,serikali imekuwa ikizungumza na wananchi ili waweze kupisha utunzaji wa mazingira katika eneo hilo na wanaojiandikisha kwa hiari ndio wanaohamishwa .

Siku moja baada ya kuibuka taarifa za vurugu Loliondo, wakati akilihutubia Bunge mjini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema hakuna mapigano katika eneo hilo .

Majaliwa alisema Serikali inaweka alama za mipaka ya eneo la hifadhi ya Loliondo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500 kutoka sehemu iliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu.

"Kilichotokea hasa ni magari ya Serikali kupita katika baadhi ya vijiji vya Loliondo yakienda kuweka minara. Ndipo baadhi ya wakazi ambao hawakufahamu hatua hiyo wakakusanyika ili kujadili suala hilo," alisema Bw Majaliwa ambaye alikuwa akitoa taarifa ya serikali baada ya kusambazwa kwa video hizo.

"Wakati wa mkutano wao, baadhi ya watu waliandamana wakidhani kwamba watafukuzwa'.

Alitoa hakikisho kuwa hakuna mtu atakayefukuzwa Loliondo .

Pia Simon Sirro, Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Tanzania siku ya Jumatatu alionya na kusema, "Zoezi hili la kuweka alama za mipaka linaloendelea Loliondo ni zoezi la kisheria linalopaswa kuheshimiwa na watu wote, wanaochochea jamii zinazoishi katika eneo hili waache kufanya hivyo.

Tutahakikisha amani inakuwepo na tutawashughulikia wale wanaojaribu kwenda kinyume na sheria. Uwekaji mipaka wa eneo hilo ulikuwa kwa maslahi ya nchi na tutahakikisha kuwa kuna amani katika mchakato huo.'

Majeruhi walikimbilia Kenya?

Serikali ya Tanzania ilipuuzilia mbali ripoti za Mbunge wa Ngorongoro Emmanuel Ole Shangai kwamba baadhi ya raia wake walikimbia nje ya nchi kutafuta matibabu.

Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa alisema "Serikali ya Tanzania haina taarifa za wanaodai kutibiwa Kenya, tunashughulika na watu walio ndani ya mipaka yetu pekee. Wanaodai kupata matibabu kwa majirani zetu wajue tuna kila kitu na hawana sababu za kwenda nje ya nchi.