Rais Samia amuhamisha Mtendaji Mkuu wa Wizara inayosimamia Loliondo na Ngorongoro kufuatia mgogoro

Muhtasari

•Ingawa taarifa ya Ikulu haijasema sababu za mabadiliko ni nini, baadhi ya maoni ya watu yanahusisha na kile kinachoendelea huko Loliondo na Ngorongoro.

•Serikali ya Tanzania inasema inaendelea kuhamasisha mamia ya familia zingine kuondoka kwa hiyari katika eneo la Ngorongoro

Image: Uhurumedia

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amemuhamisha Katibu mkuu wa Wizara ya Utalii na Maliasili, Dkt. Francis Michael kwenda wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuchukua nafasi ya Eliamani Sedoyeka aliyehamishiwa wizara ya Utalii na Maliasili.

Ingawa, taarifa ya Ikulu, kuhusu mabadiliko hayo haijasema sababu za mabadiliko ni nini, baadhi ya maoni ya watu yanahusisha na kile kinachoendelea huko Loliondo na Ngorongoro.

Michael alikuwa mtendaji mkuu wa wizara ya maliasili na Utalii, inayosimamia masuala ya hifadhi za nchi hiyo ikiwemo ya Ngorongoro na Pori Tengefu Loliondo, kaskazini mwa Tanzania, zilizoibua wasiwasi wa kiusalama hivi karibuni.

Mzozo kati ya wakazi wa Loliondo na mamlaka za Serikali umedumu kwa miaka karibu 30, na hivi karibuni ulisababisha kifo cha Polisi mmoja, kufuatia zoezi la kuweka mipaka karibu na mpaka wa pori Tengefu Loliondo kutenganisha hifadhi na maeneo ya makazi.

Kwa mujibu wa Serikali zoezi hilo linaloendeshwa kwa kufuata sheria, linalenga kunusuru uhifadhi ndani ya hifadhi, ndani ya Pori Tengefu Loliondo, na ndani ya mfumo ikolojia wa Serengeti na pia kunusuru utalii katika mfumo ikolojia huo.

Kundi la kwanza la familia 27 za jamii ya kimasai waliokuwa wanaishi ndani yahifadhi ya Ngorongoro limewasili jana mkoani Tanga kuanza maisha mapya ili kunusuru hifadhi hiyo dhidi ya kuongezeka kwa shughuli za binadamu.

Serikali ya Tanzania inasema inaendelea kuhamasisha mamia ya familia zingine kuondoka kwa hiyari katika eneo hilo la Ngorongoro, zoezi lililowahi kukutana na ukinzani mara kadhaa.