Sri Lanka: Waandamanaji wakataa kuondoka kwenye ikulu licha ya rais Rajapaksa kutangaza kujiuzulu

Rais Gotabaya Rajapaksa alisema atajiuzulu tarehe 13 Julai

Muhtasari

•Waandamanaji wamesema hawataondoka na wataendelea kushikilia makaazi ya rais na waziri mkuu wa Sri Lanka hadi viongozi wote wawili watakapojiuzulu rasmi.

•Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe alisema atajiuzulu kufuatia maandamano ya Jumamosi, ambapo makazi yake ya binafsi yalichomwa moto.

Baadhi ya waandamanaji wakiwa kwenye moja ya vyumba vya makazi ya rais Gotabaya Rajapaksa
Baadhi ya waandamanaji wakiwa kwenye moja ya vyumba vya makazi ya rais Gotabaya Rajapaksa
Image: BBC

Waandamanaji wamesema hawataondoka na wataendelea kushikilia makaazi ya rais na waziri mkuu wa Sri Lanka hadi viongozi wote wawili watakapojiuzulu rasmi.

Rais Gotabaya Rajapaksa alisema atajiuzulu tarehe 13 Julai, kulingana na tangazo lililotolewa na spika wa bunge siku ya Jumamosi. Lakini rais mwenyewe hajaonekana au kutoa taarifa kwa umma.

Maelfu walifika Colombo Jumamosi wakimtaka ajiuzulu baada ya miezi kadhaa ya maandamano. Rais amelaumiwa kwa usimamizi mbaya wa uchumi wa nchi, ambao umesababisha uhaba wa chakula, mafuta na dawa kwa miezi kadhaa.

Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe pia alisema atajiuzulu kufuatia maandamano ya Jumamosi, ambapo makazi yake ya binafsi yalichomwa moto. Pamoja na kutangazwa kuachia ngazi, lakini waandamanaji wanasalia na mashaka kuhusu nia ya viongozi hao.

Jumamosi maelfu ya waandamanaji walivamia makazi rasmi ya waziri mkuu na kuchoma moto nyumba yake.

Si Waziri Mkuu wala rais waliokuwa kwenye majengo wakati huo yakivamiwa. Mamia kwa maelfu waliwasili katika mji mkuu wa Colombo, wakimtaka Bw Rajapaksa ajiuzulu baada ya miezi kadhaa ya maandamano kuhusu hali mbaya na usimamizi mbovu wa kiuchumi.

Bw Rajapaksa atajiuzulu tarehe 13 Julai. Waziri Mkuu Wickremesinghe amekubali kujiuzulu pia. Spika wa bunge alisema rais ameamua kujiuzulu "ili kuhakikisha makabidhiano ya amani ya mamlaka" na kutoa wito kwa umma "kuheshimu sheria". Tangazo hilo liliibua furaha na kupigwa kwa mafataki ya sherehe katika jiji hilo.

Mmoja wa waandamanaji, Fiona Sirmana, ambaye alikuwa akiandamana kwenye nyumba ya rais, alisema ni wakati wa "kuwaondoa rais na waziri mkuu na kuwa na enzi mpya kwa Sri Lanka".

"Ninasikitika hawakujiuzulu mapema kwa sababu kama wangeondoka mapema kusingekuwa na uharibifu wowote," aliiambia Reuters.

Makumi ya watu walijeruhiwa katika maandamano ya Jumamosi, na msemaji wa hospitali kuu ya Colombo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu watatu walikuwa wakitibiwa majeraha ya risasi.

Sri Lanka inakabiliwa na mfumuko mkubwawa bei na inatatizika kuagiza chakula, mafuta na dawa kutoka nje kutokana na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi nchini humo kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 70.