Mikoa ya kusini mwa Tanzania imekumbwa na ugonjwa wa ajabu usiofahamika, ambao usababisha watu kutokwa damu puani na kuanguka.
Rais wa taifa hilo, Samia Suluhu amekiri kuwepo kwa ugonjwa huo leo wakati akizungumza na viongozi wa dini katika Mkutano mkuu wa 20 wa Shirikisho la mabaraza ya maaskofu wa Kanisa Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA unaofanyika jijii Dar es Salaam.
'nilikuwa nazungumza na waziri mkuu juzi, ametoka ziara kule mikoa ya kusini, Lindi ananiambia ameona kuna maradhi yameingia, wanadamu wanatokwa tu na damu za pua na wanadondoka', alisema Rais Samia
Rais Samia hakusema ni watu wangapi mpaka sasa wameathirika na haijulikani ni aina gani ya ugonjwa uliolikumba eneo hilo liloloko mpakani na nchi ya Msumbiji.
'hatujui ni kitu gani, wanasayansi wataalamu wa afya wote wamehamia huko wanaangalia ni kitu gani' alisema Rais na kuongeza 'kwanini mwanadamu atokwe tu damu za pua adondoke, angekuwa mmoja wawili tungesema presha imepanda veins zimebasti (mishipa imepasuka) anatokwa damu za pua, lakini ni wengi kwa mfululizo, ni maradhi ambayo hatujawahi ona, na yote ni kwa sababu tuna haribu makazi ya viumbe kule walikoumbwa na mungu, tunawasogeza kwetu na kutuletea aina yote hiyo ya maradhi'.
Rais Samia alikuwa akizungumza kwenye mkutano huo wa AMECEA, shirkisho linaloundwa na nchi 8 ambazo ni Zambia, Malawi, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia, Eritrea na mwenyeji Tanzania, ambapo pamoja na mambo mengine umejiegemeza kwenye masuala ya utunzaji wa mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu ya binadamu.