Muigizaji maarufu wa Nigeria ahukumiwa kwa unyanyasaji kingono dhidi ya watoto

Mwaka jana, Bw Ominyika alikiri kumdhulumu mwathiriwa.

Muhtasari

•Kesi hiyo imechukua mwaka huku upande wa mashtaka na utetezi wakiwasilisha ushahidi wao kwa nyakati tofauti mwaka jana.

•Makosa mawili ya unyanyasaji wa kijinsia yalitupiliwa mbali kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.

akipelekwa katika jela baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano
Muigizaji Olarenwaju Ominyika akipelekwa katika jela baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano

Muigizaji maarufu nchini Nigeria siku ya Alhamisi amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kumdhalilisha kingono mtoto mdogo kati ya 2013 na 2014.

Kesi hiyo imechukua mwaka huku upande wa mashtaka na utetezi wakiwasilisha ushahidi wao kwa nyakati tofauti mwaka jana.

Kulingana na mawandishi wa BBC Rhoda Odhiambo ambaye alikuwa katika mahakama ya Lagos, akiwa amevalia fulana ya manjano na suruali ya jeans nyeusi, Bw Olarenwaju Ominyika almaarufu ‘baba Ijesha’ alisimama kizimbani huku hakimu akimhukumu kifungo gerezani.

Sio tena mtu huru, lakini mfungwa hakimu aliamua kwamba anafaa kutumikia kifungo cha miaka kumi na sita kwa jumla kwa mashtaka manne ambayo alipatikana na hatia.

Lakini kwa vile angetumikia vifungo vyote kwa wakati mmoja, ikawa miaka mitano.

Makosa mawili ya unyanyasaji wa kijinsia yalitupiliwa mbali kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.

Mwaka jana, Bw Ominyika alikiri kumdhulumu mwathiriwa.

Alisema mama wa mwathiriwa alimpigia simu na kumtaka awe sehemu ya utayarishaji wa filamu, ambapo ataonekana kuwa mwanaharakati wa kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto.

Lakini hakimu alisema akiwa mtu mzima mwenye akili timamu, hakupaswa kumdhulumu mtoto, hata kama ni kwa ajili ya kuigiza.

Mwathiriwa na mamake hawakuwa mahakamani wakati uamuzi huo unasomwa.

Wanaharakati wa haki za wanawake na watoto wanasema uamuzi huo utakuwa mfano kwa yeyote anayenuia kumdhulumu mtoto.

Hata hivyo, mawakili wake wanapanga kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.