Ukraine na Urusi ziko tayari ‘kutia saini mkataba wa nafaka'

Muhtasari

• Uvamizi huo ulipelekea bei za vyakula kupanda, kwa hivyo mpango wa kufungua bandari za Ukraine ni muhimu.

Image: Reuters

Uturuki inasema makubaliano yamefikiwa na Urusi kuruhusu Ukraine kuanza tena mauzo ya nafaka kupitia Bahari Nyeusi.

Mkataba huo utasainiwa Ijumaa huko Istanbul na Ukraine, Urusi, Uturuki na Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres.

Uhaba wa nafaka za Ukraine duniani tangu uvamizi wa Urusi tarehe 24 Februari umewaacha mamilioni ya watu katika hatari ya njaa.

Uvamizi huo ulipelekea bei za vyakula kupanda, kwa hivyo mpango wa kufungua bandari za Ukraine ni muhimu. Tani milioni 20 za nafaka zimekwama kwenye maghala huko Odesa.

Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine ilithibitisha kuwa duru nyingine ya mazungumzo inayoongozwa na Umoja wa Mataifa ya kuzuia uuzaji wa nafaka nje ya nchi itafanyika siku ya Ijumaa nchini Uturuki - na mkataba "unaweza kusainiwa".

Lakini mbunge mmoja wa Ukraine aliye karibu na mazungumzo hayo alitoa tahadhari juu ya mpango huo.

"Bado hatuna makubaliano," Mbunge wa Odesa Oleksiy Honcharenko aliambia kipindi cha World Tonight cha BBC Radio 4. "Hatuwaamini Warusi hata kidogo. Kwa hivyo tusubiri hadi kesho(leo ijumaa) kwa uamuzi wa mwisho na kwamba hakutakuwa na pingamizi kutoka kwa Warusi na mabadiliko ya dakika za mwisho."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilikaribisha mpango huo uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa, lakini ilisema inalenga katika kuiwajibisha Urusi kwa kuutekeleza.

"Hatupaswi kamwe kuwa katika nafasi hii kwanza. Huu ulikuwa uamuzi wa makusudi kwa upande wa Shirikisho la Urusi kumiliki chakula," alisema msemaji wa idara hiyo Ned Price.