(Video) Tanzania yapiga marufuku mahubiri na biashara ndani ya mabasi ya masafa marefu

Mkurugenzi wa magari ya usafiri ardhini nchini humo alisema basi lolote litakalokiuka marufuku hiyo litapewa adhabu kali

Muhtasari

• "Kwa hiyo tunasisitiza biashara kwenye basi, marufuku, Wale wenye kutoa mahubiri kwenye mabasi marufuku, ni kanuni!” alisema bwana Suluo.

Biashara ya dini na mahubiri kwenye mitaa na ndani ya magari ya uchukuzi wa umma ni kero ambalo limechukuza wasafiri wengi kwa muda sasa, haswa wale ambao wamepata kutumia magari ya uchukuzi wa umma yanayofanya safari ndefu kutoka mji mmoja kuelekea mwingine kuvuka kaunti na majimbo kadhaa.

 Kero hili si tu humu nchini Kenya bali hata nchini Tanzania limekithiri mno, kiasi kwamba sasa mamlaka husika zimepiga marufuku visa kama hivyo vya mahubiri kweney magari ya uchukuzi wa umma.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini nchini humo (LATRA) imepiga marufuku shughuli hizo za mahubiri na kufanya biashara kwenye mabasi ya abiria ili kuondoa mali kwa wasafiri.

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habibu Suluo ametangaza marufuku hiyo jana Julai 26 alipozungumza na waziri wa habari ambapo amesema mabasi yatayoruhusu huduma hizo yatatozwa faini.

“Utakuta watu wanaingia kwenye mabasi kufanya biashara. Watu wanaingia kwenye mabasi wanahubiri, mambo ya dini, kwa kweli kanuni zetu zimekataza. Tunakataza kwa sababu ni vitu ambavyo si mahali pake. Na pia unapopanda labda kwenye basi ukafanya biashara, ikatokea umepata madhara kwenye biashara ile, itakuwa ni kosa. Kwa hiyo tunasisitiza biashara kwenye basi, marufuku. Wale wenye kutoa mahubiri kwenye mabasi marufuku, ni kanuni!” alisema bwana Suluo.

Alisema kwamba watakuwa na namba zote za magari na gari litakaloruhusu marufuku hiyo kukiuka litapigwa faini kubwa sana.

Marufuku hii ilipokelewa kwa njia mbalimbali huku wengi wakionekana kuishabikia kwa kusema kwamab unakuta mtu amechukua gari la masafa marefu ambapo anataka kujituliza kwa kulala angalau safarini lakini ghafla panachipuka mhubiri ambaye anawahubiria safarini tena kwa kelele za kero mpaka kuchukiza.

Wengine walisema kwamba vingi vya vyakula vinavyouzwa safarini huenda havijaafikia viwango vizuri vya usafi na mtu anapouziwa vikimharibikia tumbu huwa ni tatizo kwa sababu hakuna wa kumlaumu kwani yule mchuuzi tayari alishashuka na kuingia gari lingine kuendeleza kuuza vyakula ambavyo aghalabu husababisha magonjwa kama kipindupindu na mengine yatokanayo na kula vyakula chafu.