Kwa nini Iran inawanyonga wanawake wengi kuliko nchi nyingine yoyote?

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema Iran inaendeleza msururu wa watu kunyongwa.

Muhtasari

• Idadi ndogo inaaminika kuuawa kwa kufanya mapenzi nje ya ndoa.

• Wanawake 106 walinyongwa kwa makosa ya mauaji na 96 kwa tuhuma za uhalifu wa dawa za kulevya.

 

Wanawake hawa sita ni miongoni mwa zaidi ya 200 ambao wamenyongwa tangu mwanzoni mwa karne hii
Wanawake hawa sita ni miongoni mwa zaidi ya 200 ambao wamenyongwa tangu mwanzoni mwa karne hii
Image: BBC

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema Iran inaendeleza msururu wa watu kunyongwa. Katika wiki ya mwisho ya Julai pekee, watu 32 waliuawa, wakiwemo wanawake watatu walionyongwa kwa kuwaua waume zao.

"Hakuna kifungo cha jela kwa mauaji [nchini Iran]. Unaweza kusamehe au kutekeleza," anasema Roya Boroumand, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea haki za binadamu la Iran la Abdorrahman Borouand Center, lililoko Marekani.

Wakati mataifa mengine yanawanyonga watu zaidi ya Iran, hakuna mahali pengine ambapo wanawake wengi huuawa, kulingana na takwimu za kila mwaka za Amnesty International. Lakini kwa nini, Iran inawanyonga wanawake?

Adhabu ya kifo

Mbali na wanawake watatu waliouawa wiki iliyopita, wengine sita waliuawa katika miezi sita ya kwanza ya mwaka kulingana na Kituo cha Abdorrahman Boroumand.

Ni kweli kwamba idadi kubwa ya watu wanaonyongwa nchini ni wanaume, lakini wanawake hawa tisa wanaongezwa kwenye idadi inayoongezeka. "Kati ya 2000 na 2022, tumerekodi kunyongwa kwa takribani wanawake 233," Boroumand aliiambia BBC.

"Wanawake 106 walinyongwa kwa makosa ya mauaji na 96 kwa tuhuma za uhalifu wa dawa za kulevya," anaongeza.

Idadi ndogo inaaminika kuuawa kwa kufanya mapenzi nje ya ndoa. Boroumand anasema ni takriban 15% tu ya visa hivi vilitangazwa rasmi - tunajua kuhusu kisa kingine kutoka kwa wafungwa wa kisiasa au kutoka kwa maafisa ambao walivujisha taarifa bila idhini ya mamlaka.

Idadi kubwa ya watu kunyongwa kwa kiasi fulani inatokana na kushindwa kubadilika, Boroumand anasema: chini ya mfumo wa sheria wa nchi, serikali haiwezi kubadilisha hukumu ya kifo kwa mauaji - uamuzi wa kusamehe uko kwa familia ya mwathirika.

Hakuna usaidizi

Mwanaharakati wa Iran Atena Daemi alijaribu kupata afueni ya dakika za mwisho kwa mmoja wa wanawake ambaye alinyongwa kwa kumuua mumewe wiki iliyopita, mwanamke wa Afghanistan mwenye umri wa miaka 40, Sanubar Jalali.

Katika kitendo cha nadra cha msamaha, wazazi wa mvulana aliyeuawa walimsamehe muuaji baada ya kupelekwa kwenye mti.
Katika kitendo cha nadra cha msamaha, wazazi wa mvulana aliyeuawa walimsamehe muuaji baada ya kupelekwa kwenye mti.
Image: BBC

Daemi alikuwa akitarajia kufanya mazungumzo na familia ya mume wa Jalali kwa ajili ya kupata msamaha.

"Tulijaribu kutafuta familia ya mwathiriwa wa mauaji ili kuwasihi, lakini wakuu wa magereza hawakutusaidia. Walitupatia nambari ya simu ya wakili wake aliyetumwa na serikali, lakini alipuuza maombi yetu," Daemi aliiambia BBC.

"Mamlaka ya magereza wakati mwingine husaidia kuomba familia kukubali kupokea ada ya msamaha, lakini hilo halifanyiki kila wakati."

Lakini Boroumand anaweza kuangazia baadhi ya mafanikio - kufanya kazi na wanaharakati wengine anasema kumewanusuru watu wawili kunyongwa na wengine wanane kukatwa sehemu ya mwili.

Wanawake wengine wawili walionyongwa kama siku moja na Jalali, mmoja alikuwa bibi harusi mchanga ambaye aliozwa akiwa na umri wa miaka 15. Mwanamke wa tatu mara ya kwanza alikamatwa na kwa kumuua mume wake miaka mitano iliyopita.

Ulinzi dhaifu

Daemi amezuiliwa gerezani kwa miaka saba kutokana na harakati zake.

Anasema magereza ya wanawake yanakosa mahitaji ya msingi na wakati mwingine wafungwa hupigwa.

Atena Daemi anasema upendeleo wa kijinsia katika mfumo wa mahakama unafanya iwe vigumu kwa mwanamke aliyeshtakiwa kwa mauaji kuachiliwa huru.
Atena Daemi anasema upendeleo wa kijinsia katika mfumo wa mahakama unafanya iwe vigumu kwa mwanamke aliyeshtakiwa kwa mauaji kuachiliwa huru.
Image: BBC

Kesi za mahakama pia anasema mara nyingi huwa na uzito dhidi ya wanawake, kwani wanaume pekee wanaweza kuwa majaji na mawakili wengi pia ni wanaume.

Mahakama za Iran lazima zitoe wakili wa utetezi, lakini Daemi anasema hazitoi msaada mkubwa wa kisheria kwani "wengi wa mawakili hawa waliopewa kazi ni majaji au waendesha mashtaka wa zamani".

"Kujidhihirisha kuwa huna hatia si rahisi katika kesi za mauaji. Katika kesi kama hizo, maneno ya wanafamilia ya mwathiriwa yana athari zaidi kuliko ya mtuhumiwa," anasema Daemi

Mfumo dume

Mwandishi wa habari wa Iran Asieh Amini, ambaye sasa anaishi Norway, amefuatilia kwa karibu kesi ambapo wanawake huhukumiwa kifo. Anasema chanzo cha tatizo ni mfumo wa sheria wenyewe.

Familia nyingi zilikata uhusiano na wanawake waliofungwa, wanaharakati wanasema.
Familia nyingi zilikata uhusiano na wanawake waliofungwa, wanaharakati wanasema.

"Kulingana na sheria, baba na babu wa baba ndio wakuu wa familia na wanaweza kuamua hatima ya binti zao, ikiwa ni pamoja na ndoa," Amini aliambia BBC.

Hii ina maana kwamba wasichana ambao wanalazimishwa kuolewa wanaweza kukabiliwa na matatizo makubwa, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa nyumbani, na ni vigumu kupata talaka kutoka kwa mahakama za Iran, anaongeza.

Wanawake ambao wamehukumiwa kifo mara nyingi hukosa hata kuungwa mkono na wazazi wao, ambao wanaweza kudumisha kile wanachokiona kama 'heshima ya familia'.

"Katika hali hii, baadhi ya wanawake wanasalia kuwa waathirika wa ukatili milele," anasema Amini.

Wengine wanaamua kuua waume zao.

"Baadhi ya wanawake hao walikiri kuwa walifanya mauaji hayo wao wenyewe au kuna mtu aliyewasaidia.

Lakini karibu wote walisisitiza kuwa iwapo kungekuwa na njia ya kuwaunga mkono dhidi ya ukatili wanaoupata, wasingeweza kufanya kosa la mauaji. " anasema.

 

Asieh Amini analaumu sheria za kidini na jamii ya mfumo dume kwa kunyongwa kwa wanawake nchini Iran
Asieh Amini analaumu sheria za kidini na jamii ya mfumo dume kwa kunyongwa kwa wanawake nchini Iran
Image: BBC

Unyongaji wa watoto

Amini anatoa mfano wa jinsi baadhi ya wanawake wanavyoshughulikiwa na mahakama kama vile kisa cha msichana Atefeh Sahaleh mwenye umri wa miaka 16 aliyenyanyaswa kijinsia na wanaume kadhaa.

Badala ya kutafuta haki kwa msichana huyo, majaji waliamua mwaka 2004 kwamba alikuwa amefanya ngono nje ya ndoa.

"Alihukumiwa kifo kwa kukiri kufanya mapenzi na baadhi ya wanaume, wakati ukweli ni kwamba alibakwa," anasema Amini.

Anaeleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Adhabu za Kiislamu nchini Iran, ikiwa mtu asiye na mume atakiri kufanya mapenzi nje ya ndoa, atahukumiwa kuchapwa viboko 100. Na akirudia kitendo hicho mara tatu, anaweza kuhukumiwa kifo akipatikana na hatia mara ya nne.

"Lakini kwa upande wa Atefeh hata hiyo sheria isiyo ya kibinadamu haikutumika, maana nilikuta amechapwa viboko 100 mara mbili tu kabla ya hakimu kutoa hukumu ya kunyongwa," anasema Amini.

"Kwa mara ya nne, jaji mwenyewe ambaye jina lake lilikuwa Haji Rezaei, alimvisha Atefeh kamba shingoni."

Asieh Amini analaumu sheria za kidini na jamii ya mfumo dume kwa kunyongwa kwa wanawake nchini Iran
Asieh Amini analaumu sheria za kidini na jamii ya mfumo dume kwa kunyongwa kwa wanawake nchini Iran
Image: BBC

Mohammadi anaamini kuwa familia ya mume aliyeuawa iliweka shinikizo kubwa kwa mtoto wa kiume na jamaa zake kuzingatia "heshima ya familia".

Chombo cha vitisho

Amini anahoji ubaguzi katika sheria, mahakama na utamaduni "unachangia kuwafikisha wanawake hawa katika hatua ya mwisho, na kuwafanya wahalifu au waathiriwa," lakini hana uhakika wa nini cha kufanya kuhusu mauaji haya ya haraka.

"Kwa kweli sikuwahi kuelewa katika kipindi cha miaka ambayo nilifuata kesi hizi kutoka gerezani hadi gerezani, jinsi serikali ya Irani inanufaika na adhabu hiyo ya kikatili," anasema.

Boroumand ana nadharia ingawa.

Nje ya Iran, kumekuwa na maandamano mengi dhidi ya matumizi ya Iran ya adhabu ya kifo.
Nje ya Iran, kumekuwa na maandamano mengi dhidi ya matumizi ya Iran ya adhabu ya kifo.

Magereza ya Iran sasa yamejaa wafungwa wa kisiasa na watumiaji wa dawa za kulevya, na ili kupunguza msongamano katika jela, anadhani maafisa wanashinikiza jamaa za watu waliouawa kuharakisha uamuzi wao - huruma au kifo.

Boroumand anahofia hii inasababisha wengi zaidi kunyongwa. Pia anashuku kuwa mamlaka ina nia potofu ya adhabu kali.

"Hivi karibuni mwanaume mmoja alikatwa mkono huko Tehran. Wanaleta wafungwa kutoka miji mingine kufanya ukataji wa viungo, anasema.

"Hawaitangazi lakini wanaifanya kwa njia ambayo habari kuhusu adhabu itaenea katika jamii pana, na kuleta hofu miongoni mwa wanaharakati."

Serikali ya Iran haijajibu ombi la BBC la kutaka maoni yake, lakini mahakama ya Iran hapo awali ilisema kuwa hukumu hiyo ni halali na haikiuki majukumu ya kimataifa ya Iran (mikataba iliyosainiwa). Serikali ya Iran imekanusha mara kwa mara ripoti za kuteswa na wati kulazimishwa kukiri.