Polisi watano wauawa Mashariki ya DR Congo

Magari yalichomwa moto na silaha 8 zilipatikana kutoka kwa washambuliaji.

Image: AFP

Kwa mujibu wa wakazi wa Butembo, polisi walipelekwa majira ya asubuhi ya leo kurudisha amani na utulivu katika viunga vya mji ambapo baadhi ya waandamanaji wenye hasira waliwageukia polisi.

Mapema leo msemaji wa jeshi aliiambia BBC kuwa idadi ya waliouawa ni maafisa 5, magari yalichomwa moto na kwamba silaha 8 zilipatikana kutoka kwa washambuliaji.

Wapiganaji wa eneo hilo wanaojulikana kama Mai Mai Baraka wanalaumiwa kwa tukio la leo.

Tukio la leo linajiri siku chache baada ya Allied Democratic Forces, kundi katili lililojihami na linalofungamana na kundi la Jihadi la Islamic State, kushambulia gereza kuu la Kakwangura huko Butembo.

Kundi la IS lilidai kuhusika na tukio hilo la gerezani likisema lilifanywa kuwaachilia huru makumi ya wafungwa Waislamu.

Waasi wa ADF walitoka Uganda, lakini kwa miaka 27 iliyopita mashambulizi yao mengi yamekuwa yakilenga raia mashariki mwa DRC.

Vyombo vya usalama vya eneo hilo vinasema kuwa ADF walisaidiwa na makundi ya wenyejiyenye silaha walipovamia gereza hilo.

Roger Moya, naibu meya wa Butembo alisema takriban watu 250 waliotoroka wamekamatwa tena na vikosi vya usalama hadi kufikia sasa. Lakini zaidi yawafungwa 800 waliotoroka wakati wa uvunjaji wa gereza bado wako huru.