Mtoto aliyezaliwa kutokana na ubakaji amsaidia mama yake kupata haki

Ubakaji huo ulifanyika kwa muda wa miezi sita

Muhtasari

•Mwanamke huyo alibakwa kwa zaidi ya miezi sita na wanaume wawili alipokuwa na umri wa miaka 12 pekee. 

•Daktari alikataa kutoa mimba kwa sababu ya afya yake dhaifu na umri mdogo.

Mwanamke huyo alisema mwanawe alikuwa akimuuliza mara kwa mara kuhusu babake
Mwanamke huyo alisema mwanawe alikuwa akimuuliza mara kwa mara kuhusu babake
Image: MAKTABA

Takriban miongo mitatu baada ya mwanamke wa Kihindi kubakwa mara kwa mara na ndugu wawili, hatimaye sasa ana matumaini kupata haki na anayemsaidia katika harakati zake ni mtoto wa kiume aliyezaliwa kutokana na kushambuliwa huko kingono.

Mwanamke huyo katika jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh alibakwa kwa zaidi ya miezi sita na wanaume wawili alipokuwa na umri wa miaka 12 pekee. Mtoto wake, ambaye alimtoa kwa ajili ya kuasili lna kurudishwa kwake miaka 13 baadaye, alimhimiza afungue kesi dhidi ya wanaodaiwa kumbaka.

Siku kumi zilizopita, polisi walimkamata mmoja wa washtakiwa na Jumatano, mtu wa pili pia aliwekwa chini ya ulinzi. "Tukio hilo ni la zamani sana lakini majeraha ambayo yalisababisha bado hayajapona," mwanamke huyo aliambia BBC. "Imeleta kumbukumbu ya maisha yangu na ninakumbuka wakati huo tena na tena." Maelfu ya visa vya unyanyasaji wa kingono kwa watoto huripotiwa nchini India kila mwaka. Mwaka 2020 mwaka ambao takwimu rasmi ya uhalifu zipo inaonesha kesi 47,000 zilisajiliwa chini ya Sheria ya India ya Ulinzi wa Watoto dhidi ya Makosa ya Kujamiiana (Pocso).

Wanaharakati wanasema kesi nyingi zaidi haziripotiwi kwa sababu watoto ni wadogo sana kuelewa kinachoendelea kwao au wanaogopa sana kusema.

Familia pia mara nyingi husitasita kuripoti unyanyasaji kama huo kwa sababu ya unyanyapaa au ikiwa wahusika wanajulikana.

'Walinitia hofu moyoni'

Mwathiriwa wa ubakaji katika mji wa Uttar Pradesh, ambaye jina lake haliwezi kuwekwa wazi chini ya sheria za India, alisema ubakaji huo ulifanyika mwaka 1994 katika mji wa Shahjahanpur.

Mshtakiwa, Mohammed Razi na kaka yake Naqi Hasan, waliishi katika mtaa huo na walikuwa wakiruka ukuta wa mpaka wa nyumba yake na kumshambulia kila alipokuwa peke yake. Mimba hiyo iligunduliwa pale tu afya yake ilipoanza kuzorota na dada yake kumpeleka kwa daktari.

Daktari alikataa kutoa mimba kwa sababu ya afya yake dhaifu na umri mdogo. Mara tu baada ya kuzaliwa, mtoto alitolewa kwa ajili ya mtu anayetaka kuasili mtoto.

"Niliteseka sana kwa ajili ya mtoto huyu lakini sikupata hata nafasi ya kumuona usoni. Nilipomuuliza mama yangu alisema, 'sasa utapata nafasi ya pili maishani'." Mwathiriwa na familia yake hawakuandikisha malalamiko polisi kwa sababu mwanamke huyo alisema aliishi kwa hofu ya washtakiwa

Walitishia kuua familia yangu na kuchoma nyumba yetu ikiwa nitamwambia mtu yeyote kuhusu ubakaji huo," alisema. "Ndoto yangu ilikuwa kukua na kujiunga na polisi, lakini kwa sababu ya watu hao wawili, ndoto zangu zote zilifikia mwisho. Nilikosa shule, sikuweza kusoma."

Mwanamke huyo na familia yake baadaye walihamia wilaya ya Rampur ili kuepuka kumbukumbu za majeraha zinazohusiana na nyumba yao ya awali. Mnamo 2000, aliolewa na kupata mtoto wa pili. Anasema alitarajia sura hii mpya ingemsaidia kusahau yaliyopita, lakini miaka sita ya ndoa, mumewe aligundua kuhusu ubakaji na akamlaumu kwa hilo.

Baadayealimfukuza pamoja na mwanawe, alienda kuishi na dada yake na familia yake.

Mtoto kuutafuta ukweli

Mtoto wake wa kwanza wa kiume, ambaye alitolewa ili alelewe na familia nyingine, pia alikabiliwa na ubaguzi mwingi kwa sababu ya utambulisho wake.

Mama yake alisema alikua akisikia kwa majirani zake kuwa yeye sio mtoto wa wazazi anaoishi nao na ndipo alipogundua kuwa ameasiliwa.

Miaka kumi na tatu baada ya mama na mwana kutengana, wazazi walezi walimrudisha mtoto kwa mama yake.

Lakini mtoto alitamani kujua baba yake ni nani. Hakuwa na jina la ukoo huko India, kwa kawaida ni jina la baba na watoto walimdhihaki shuleni.

Mara kwa mara alikuwa akimuuliza mama yake maswali kuhusu malezi ya uzazi wake na kutopata jibu jambo lililomkera sana. Mwanamke huyo alisema mtoto wake alimwambia kwamba "hawezi kuishi maisha haya yasiyo na jina" na akatishia kujiua ikiwa atafichua jina la babake.

Awali, alisema, alimkemea kwa kuuliza maswali, lakini hatimaye, alikubali na kumwambia ukweli.

Badala ya kushtushwa, mtoto huyo aligeuka kuwa msaada wake mkuu, akimwambia kwamba alipaswa "kupigana vita hivi na kumfundisha mshtakiwa somo."

"Ikiwa utazungumza juu ya kile kilichotokea, labda watu wengi zaidi watajitokeza pia kuzungumza. Hiyo itaimarisha kesi yetu na washtakiwa watapata adhabu. Ujumbe utatumwa kwa jamii kwamba hakuna mtu anayeweza kuokoka baada ya kufanya uhalifu."

Kupigania haki

Kwa kutiwa moyo na mtoto wake, mwanamke huyo alitembelea tena Shahjahanpur mwaka 2020, lakini alipata shida kufungua kesi dhidi ya mshtakiwa.

Polisi walikataa kufungua malalamiko yake kwa sababu yalikuwa ya zamani sana, alifika kwa wakili, wakili huyo pia alisitasita, akisema itakuwa vigumu kupigania kesi ambayo ilikuwa ya takriban miongo mitatu tangu ilipoanza.

Eneo alilokuwa akiishi akiwa mtoto lilikuwa limebadilika zaidi ya kutambulika hakuweza hata kupata nyumba yake ya zamani na washtakiwa hawakuweza kufuatiliwa.

"Ungethibitishaje mahali ulipoishi miongo mitatu nyuma na ndipo ulipobakwa?" wakili wake aliuliza.

"Nilimwambia, tutakuletea ushahidi, chukua kesi yetu," alisema.

Wakili huyo aliwasilisha rufaa mahakamani na kwa amri ya hakimu mkuu wa mahakama ya Shahjahanpur, kesi ilisajiliwa dhidi ya washtakiwa hao wawili mnamo Machi 2021.

“Niliwapata nikazungumza nao kwa simu, wakanitambua na kuniuliza kwa nini bado sijafa,” anasema mwanamke huyo. "Nilisema, sasa ni zamu yako kufa."

Ushahidi na kukamatwa

Ingawa washtakiwa walikuwa wamefuatiliwa, hakukuwa na ushahidi wa kuwaunganisha na uhalifu huo. Polisi wanasema kuwa ushahidi sasa umetoka katika vipimo vya DNA vilivyochukuliwa mwezi Februari.

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi wa Shahjahanpur (SSP) S Anand aliambia BBC, "Kesi hii haikutarajiwa kabisa. Mwanamke huyo alipojitokeza na kufungua kesi, tulishangaa sana. Lakini tulichukua uamuzi wa kupima sampuli za DNA za mtoto wake."

Inspekta Dharmendra Kumar Gupta, ambaye amekuwa akichunguza kesi hiyo kwa mwaka uliopita, alisema, "Baadaye tulikusanya sampuli za DNA kutoka kwa washtakiwa na kuzifanyia uchunguzi. Mmoja wao alilingana na sampuli za DNA za mtoto."

Mnamo tarehe 31 Julai, mmoja wa washtakiwa alikamatwa na Jumatano, polisi walisema walikuwa na mtu wa pili pia kizuizini. Washtakiwa hao bado hawajazungumza lolote kuhusu tuhuma zinazowakabili.

Mwanamke huyo anasema anataka simulizi yake iwatie moyo wengine kujitokeza na kuripoti uhalifu uliofanywa dhidi yao. "Watu wanakaa kimya. Mimi pia nilikaa kimya na nilifikiri kwamba hii ndiyo ilikuwa imeandikwa katika hatima yangu. Lakini hakuna kitu kama hicho. Ni lazima tuende polisi kwahiyo hakuna mtu yeyote anayepaswa kuvumilia kile tulichopaswa kuvumilia."

Kuhusu mtoto wake, anasema anafurahi kuwa washtakiwa wamekamatwa.