Tanzania yaonya dhidi ya kusambaza maudhui yanayounga mkono mapenzi ya jinsia moja

Muhtasari

•Waziri wa mawasiliano alisema ni kosa kisheria nchini Tanzania kwa mtu yeyote kusambaza maudhui hayo hata kama yanalenga kuelimisha.

Image: GETTY IMAGES

Serikali ya Tanzania imetoa onyo kwa wanaojihusisha na kusambaza maudhui mitandaoni ikiwemo video fupi zinazohimiza uhusiano wa jinsia moja.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliyasema hayo jana Jumapili  jijini Dar es Salaam ambapo alisema kuwa  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilibaini kuwa baadhi ya watazamaji wa maudhui ya kulipia mtandaoni wamekuwa wakitazama na kusambaza maudhui hayo zikiwemo video kwenye mitandao ya kijamii. 

Nape alieleza kuwa uwepo wa huduma hizo zinazopatikana ulimwenguni zinawafanya watu kupokea tamaduni, mila na desturi kupitia picha jongefu wanazoangalia mtandaoni baada ya kulipia. 

Alisema ni kosa kisheria nchini Tanzania kwa mtu yeyote kusambaza maudhui hayo hata kama yanalenga kuelimisha, badala yake wanapotumiwa video hizo wafute na si kuzisambaza. 

Aidha alisema Serikali imepanga kuwachukua hatua kali kwa wanaoongoza makundi ya mitandao ya kijamii ambao wanachama wao wamekuwa wakishawishi kitendo hicho kwa kusambaza maudhui hayo. 

“Kiujumla anga letu la mtandao liko salama kwani TCRA wapo kazini kuhakikisha kuwa tunaendelea kuwa salama na hata inapotokea kuna maudhui hasi na yanayokiuka sheria, inachukua hatua stahiki kwa wanaohusika kwa kushirikiana na vyombo vya dola hasa jeshi la polisi,” alisema Nape. 

Nape amewahas wazazi, walimu na walezi kuwa wana wajibu wa kuwalinda watoto kutokana na maudhui yasiyofaa hasa yanayorushwa kwenye mitandao ya kijamii.