Maelfu wanamtetea profesa aliyemtakia Malkia Elizabeth II kifo kibaya na cha uchungu

Profesa Uju Anya aliandika maneno makali dhidi ya malkia Elizabeth kwenye Tweeter yake akimtaja kama mtu mbaya sana anayestahili adhabu kali ya kifo

Muhtasari

• Jarida la New York Times liliripoti kwamba maelfu ya wasomi na wanafunzi wametia saini takribani mara 4000 kumtetea Anya dhidi ya vitisho kutoka uongozi wa chuo cha Mellon anakofunza.

profesa Uju Anya aliyemtakia malkia Elizabeth 2 atetewa
profesa Uju Anya aliyemtakia malkia Elizabeth 2 atetewa
Image: Twitter, maktaba

Wiki iliyopita dunia ilipokea taarifa za tanzia kutoka kasri la Buckingham nchini Uingereza kufuatia kifo cha malkia Elizabeth wa pili.

Watu wengi kutoka matabaka yote ulimwenguni walijumuika kutuma risala za rambi rambi huku wakimtakia pumziko la amani.

Ila kulikuwepo na Tweet moja ambayo kabla ya kufutwa na mwenyewe kweney mtandao wa Twitter, ilikuwa imesambazwa pakubwa. Tweet hiyo ilikuwa ni ya profesa mmoja mhadhiri wa chuo kikuu cha Carnegie Mellon, kwa jina Uju Anya.

Msomi huyo kutokea Nigeria alizungumziwa sana baada ya kuenda kinyume na msemo, Marehemu hasemwi vibaya. Kwake, ilikuwa ni fursa nyingine ya kumtakia mabaya sana akhera malkia Elizabeth wa pili.

“Nilisikia mfalme mkuu wa himaya ya mauaji na ubakaji hatimaye amekufa. Namtakia maumivu yake yawe makali,” profesa Uju Anya aliandika kwenye Twitter.

Kutokana na matamshi haya, msomi huyo alipokea masimango mengi kutoka kwa maelfu ya watu kote ulimwenguni walioonekana kuchukizwa na cheche zake kali dhidi ya hayati malkia Elizabeth aliyefariki na umri wa miaka 96.

Sasa jarida la New York Times limeibuka na habari mpya kwamba profesa huyo amepokea uungwaji mkono na watu wengi zaidi ambao wameandika barua ya kumuunga mkono na kusimama naye kutokana na kusema ukweli wake amabo wanasema wengi waliogopa kuusema.

“Maelfu ya wasomi na wanafunzi walitia saini ombi la kumtetea profesa wa Chuo Kikuu cha Carnegie Mellon ambaye alimtakia Malkia Elizabeth kifo "kibaya" masaa kabla ya kuaga wiki jana. Ombi linalomtetea Anya, ambalo lilikuwa limetiwa saini karibu mara 4,000 kufikia Jumatatu alasiri, linamtetea kwa kusema kwamba Malkia Elizabeth II alikuwa "mkoloni wa kihalisi."” Jarida la New York Times liliripoti.

Wasomi na wanafunzi hao walisimama kidete kutetea profesa Anya kutokana na hatua ya chuo hicho kutaka kumfuta kazi huku wakisema kwamba hakuzungumza kwa niaba ya chuo bali matamshi yalikuwa ni fikra zake tu naye kama mwanadamu yeyote ana haki ya kuzungumza maoni yake.