Mbunge ashauri kuanzishwa kwa viwanda vya kupunguza makali ya bangi kabla kutumiwa

Alisema bangi kuna watu wakitumia wanafanya kazi vizuri zaidi kama kulima.

Muhtasari

• Wako watu wakitumia hivyo wanaweza kulima zaidi, anaweza kufanya kazi hii na mwingine anavuta tu kama sigara - Ngonyani.

Mbunge maalum ataka serikali kuhalalisha bangi
Jackline Ngonyani Mbunge maalum ataka serikali kuhalalisha bangi
Image: Facebook screengrab

Mbunge maalumu nchini Tanzania amepeleka bungeni suala la kutaka serikali ya nchi hiyo kuanzisha ujenzi wa viwanda vya bangi.

Mbunge huyo maalumu kwa jina Jackline Ngonyani alizungumza kwenye bunge akitaka serikali kuanzisha mchakato na kuwepo kwa viwanda hivyo vitakavyofanay kazi ya kuchukua bangi na kuipunguza makali kabla ya kuwapa wananchi kuitumia kadri wanavyojihisi.

Akitetea hoja yake, mbunge Ngonyani alisema kwamba nchini humo wapo watu wengi ambao wanapanda na kutumia bangi pasi na serikali kujua kwa sababu haina mifumo ya kuweza kujua mtu fulani amepanda bangi na kusema ni wakati wananchi waruhusiwe kuitumia pindi tu inapopunguzwa makali.

“Suala la bangi mimi ndio naona tatizo kubwa sana, kwa sababu bangi inalimwa hata kwenye upenuni mwa nyumba, hata bafuni mtu anaweza akalima bangi hiyo na mwisho wa siku anaitumia kimya kimya. Hatuna mifumo ya kujua nyumba hii au shamba hili lina bangi,” mbunge huyo alisema.

“Sasa basi kwa nini suala hili la bangi tusilichukue tukakaa upya tukajadiliana ili ikiwezekana bangi hii tuiprocess, na tuweze kujenga viwanda ambavyo vitapunguza makali ili bangi hii iweze kutumika kwenye maeneo mbali mbali kwa sababu wako watu wakitumia hivyo wanaweza kulima zaidi, anaweza kufanya kazi hii na mwingine anavuta tu kama sigara,” mbunge Ngonyani alitetea hoja yake kwa msisitizo.

Hakuishia hapo. Mbunge huyo alijihami vizuri na mifano hai ambapo alisema nchi kama Zimbabwe wanalima bangi na tayari wameshaipitisha kaam biashara ya kuingiza pato la taifa.

Mifano mingine aliyotolea ni Jamaica, Marekani, Korea Kaskazini na kusema nchi kama Tanzania kwani wanakwama wapi badala ya kukumbatia ukulima huu wa kuzalisha pato la taifa.

“Kwa nini sisi tusiiprocess tukapunguza makali na watu watumie kama kadri mtu anavyoona sawa sawa na sigara wanasema tumia lakini ni hatari kwa afya yako. Kwa hiyo mtu ana hiari kuitumia au kuiacha kuliko kuacha pato hili la taifa linaendelea kutokomea,” mbunge huyo alisema huku bunge zima zikipasuka vicheko.