Mwanafunzi wa umri wa miaka 17 ajifyatulia risasi, aacha barua mwili wake uchomwe

Mwanafunzi huyo alitaka majivu kusafirishwa hadi Marekani kuzikwa kando ya kaburi la babake

Muhtasari

 
• Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, baba yake Robert alifariki dunia akiwa Marekani na mwili wake haukusafirishwa Tanzania kwa ajili ya maziko bali ulizikwa huko ughaibuni.

Mwanafunzi ajiua kwa kujipiga risasi Kilimanjaro
Mwanafunzi ajiua kwa kujipiga risasi Kilimanjaro
Image: YoutubeScreengrab

Mwanafunzi wa umri wa miaka 17 amejiua kwa kujipiga risasi na kisha kuacha maagizo kwamba mwili wake usizikwe bali uchomwe.

Tukio hili liliripotiwa nchini Tanzania katika mkoa wa Kilimanjaro. Mwanafunzi huyo kwa jina Robert Meier alikuwa anasoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari St Mary Goreti iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani humo.

Kulingana na taarifa zilizosambazwa na Mwananchi Digital, kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema lilitokea usiku wa kuamkia juzi.

Maigwa alidai kuwa kabla ya mwanafunzi huyo kujiua, aliacha ujumbe wa maandishi ulisomeka mwili wake uchomwe na majivu yake yasafirishwe kwenda Marekani yakazikwe pembezoni mwa kaburi la baba yake.

Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, baba yake Robert alifariki dunia akiwa Marekani na mwili wake haukusafirishwa Tanzania kwa ajili ya maziko bali ulizikwa huko ughaibuni.

Mwanafunzi huyo alijifyatulia risasi katika upande wa kushoto wa kifua kwenye moyo na kutokea mgongoni. Alitumia bastola ya mkaazi mmoja wa maeneo hayo kwa jina Boniface Kimario ambayo jeshi la polisi lilidhibitisha ni mmiliki halali ila kwa sasa naye ameshikiliwa kwa uchunguzi zaidi.

Hayo yanajiri katika nchi Jirani miezi michache tu baada ya humu nchini mtoto wa mbunge maalumu David Ole Sankok kujiua kwa kujifyatulia risasi nyumbani kwao katika kaunti ya Narok.

Mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miaka 15 alikuwa pia ni mwanafunzo katika shule ya upili ya Kericho.