Rais wa Ukraine Zelensky ahusika katika ajali ya gari lakini 'hakujeruhiwa sana'

Muhtasari

• Gari la abiria liligongana na gari la rais na msafara wake katika mji mkuu wa Kyiv, Sergii Nykyforov alisema katika taarifa fupi.

Image: BBC

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amehusika katika ajali ya barabarani, msemaji wake amefichua.

Gari la abiria liligongana na gari la rais na msafara wake katika mji mkuu wa Kyiv, Sergii Nykyforov alisema katika taarifa fupi.

“Rais alifanyiwa uchunguzi na daktari, hakuna majeraha makubwa yaliyopatikana,” alisema.

Dereva wa gari lililogongana na msafara huo alitibiwa eneo la tukio na kukimbizwa kwenye gari la wagonjwa. 

Bw Nykyforov alisema mazingira yote ya ajali hiyo ya barabarani yalikuwa yanachunguzwa na maafisa wa kutekeleza sheria. Hakutoa maelezo zaidi.

Haya yanajiri baada ya Rais Zelensky, 44, kutembelea mji uliokombolewa  wa Izyum, kitovu muhimu cha usafirishaji kaskazini-mashariki mwa Ukraine, siku ya Jumatano.

Aliwashukuru wanajeshi walioshiriki katika mashambulizi ya haraka dhidi ya wavamizi wa Urusi, na kusimamia sherehe ya kupandisha bendera.

Katika siku za hivi karibuni, jeshi la Ukraine limerejesha sehemu kubwa ya eneo lililokaliwa, na kuwalazimu wanajeshi wa Urusi kurudi nyuma.