Kundi la Wagner: Mkuu wa mamluki Urusi arekodiwa video akisajili makurutu gerezani

Prigozhin aliwaambia wafungwa vifungo vyao vitabadilishwa ili waweze kuhudumu katika kundi lake.

Muhtasari

Ukraine aliwaonya watu wanaoweza kuajiriwa dhidi ya kutoroka na akasema ‘’ikiwa utafika Ukraine na kuamua sio kwako, tutakunyonga’’.

Kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner nchini Urusi ameonekana kwenye video zilizovuja akijaribu kusajili wafungwa kupigana nchini Ukraine.
Kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner nchini Urusi ameonekana kwenye video zilizovuja akijaribu kusajili wafungwa kupigana nchini Ukraine.
Image: LEAKED VIDEO

Mwanzilishi wa kundi la mamluki la Wagner nchini Urusi ameonekana kwenye video zilizovuja akijaribu kusajili wafungwa kupigana nchini Ukraine.

Katika picha zilizorekodiwa, zilizothibitishwa na BBC, Yevgeniy Prigozhin anaweza kuonekana akihutubia kundi kubwa la wafungwa.

Bw Prigozhin aliwaambia wafungwa vifungo vyao vitabadilishwa ili waweze kuhudumu katika kundi lake.

Video hiyo itathibitisha uvumi wa muda mrefu kwamba Urusi inatarajia kusajili wanajeshi zaidi na kujiimarisha kwa kusajili wafungwa.

Ingawa sheria za Urusi haziruhusu kubadilishwa kwa vifungo vya jela ili kutoa huduma ya mamluki, Bw Prigozhin alisisitiza kwamba ‘’hakuna mtu anayerudi gerezani’’ ikiwa atatumikia pamoja na kundi lake.

‘’Ikiwa utatumikia miezi sita (kwa kundi la Wagner), uko huru,’’ alisema.

Lakini aliwaonya watu wanaoweza kuajiriwa dhidi ya kutoroka na akasema ‘’ikiwa utafika Ukraine na kuamua sio kwako, tutakunyonga’’.

Pia aliwafahamisha wafungwa sheria za Wagner za kupiga marufuku pombe, dawa za kulevya na ‘’mahusiano ya ngono na wanawake wa eneo hilo, mimea, wanyama, wanaume – chochote’’.

Akizungumza katika kile kinachoonekana makazi yanayotumika kuwafukuza wafungwa na kuwatenganisha na watu kwa ujumla kwa kuwaweka katika eneo la mbali, mkuu wa mamluki pia aligusia matatizo ambayo Urusi imekumbana nayo katika mzozo huo wa muda mrefu, akiwaambia wafungwa kwamba ‘’hivi ni vita vikali, hata karibu na Chechnya na vingine’’.

Haijulikani ni nani alirekodi video hiyo, ilitokea lini au jinsi ilitolewa.

Lakini BBC imeweka picha hizo kwenye eneo hilo katikati mwa Jamhuri ya Mariy El nchini Urusi.

Wachambuzi walifanya hivyo kwa kufanya upekuzi wa picha ya kinyume kwenye kanisa linaloonekana nyuma ya video, na kulingana na eneo hilo hasa namba sita.

Picha ya skrini kwenye uso wa msajili pia ilipitishwa kwenye programu za utambuzi wa uso, na kurudisha matokeo chanya ya kati ya 71% na 75% na picha halisi ya Bw Prigozhin.

Kando na hilo, vyanzo vilithibitishia idhaa ya BBC ya Kirusi kwamba huenda mtu aliye kwenye video hiyo ni Bw Prigozhin.

‘’Hii ni sauti yake. Toni yake. Maneno yake na namna ya kuongea... Nina uhakika kwa asilimia 95 kuwa huyu ni yeye na huyu si mzushi,’’ chanzo kimoja kiliiambia BBC.

‘’Inafanana sana, tabia yake, na sauti yake inafanana sana,’’ mwingine alisema.

Mwenye kampuni hiyo, 61, Concord, ilikataa kukana kwamba alionekana kwenye video hiyo, ikibaini kufanana kwake ‘’kwa kutisha’’ alipozungumza na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

Yevgeniy Prigozhin na Vladimir Putin mnamo 2010
Yevgeniy Prigozhin na Vladimir Putin mnamo 2010
Image: GETTY IMAGES

Bw Prigozhin - ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi Vladimir Putin - hapo awali alikana uhusiano na kundi la Wagner, ambalo vikosi vyake vimetumwa nchini Ukraine, Syria na migogoro kadhaa ya Afrika.

Lakini katika video hiyo, tajiri wa Urusi anaweza kuonekana akiwaambia wafungwa kwamba yeye ni ‘’mwakilishi wa kampuni ya kibinafsi inayoangazia vita.’’

‘’Labda ulisikia jina – kundi la Wagner’’, anauliza kundi la wafungwa.

Alisema makurutu lazima wawe na ‘’umbo zuri la kimwili’’, kabla ya kufichua kwamba makurutu 40 wa kwanza kutoka eneo hilo huko St Petersburg walitumwa wakati wa shambulio kwenye Kituo cha Nguvu cha Vuhlehirska mashariki mwa Ukraine mwezi Juni mwaka jana.

Alisema wafungwa hao walivamia mahandaki ya Ukraine na kuwashambulia wanajeshi wa Kyiv kwa visu.

Watatu kati ya wanaume hao - ikiwa ni pamoja na mwenye umri wa miaka 52 ambaye alitumia zaidi ya miaka 30 kizuizini - waliuawa, Bw Prigozhin alisema.

Baadaye kwenye video hiyo, aliwaonya wafungwa hao ambao wote wanavalia mavazi meusi, kwamba watatarajiwa kujiua kwa mabomu ya kutupa kwa mkono iwapo watakuwa katika hatari ya kunaswa.

Asili ya kundi la Wagner haijulikani wazi, lakini inaaminika kuwa liliundwa na afisa wa zamani wa jeshi la Urusi, Dmitri Utkin.

Hapo awali BBC ilitambua uhusiano kati ya kundi hilo na Bw Prigozhin, anayejulikana kama ‘’mpishi wa Putin’’ - kinachojulikana kwa sababu alipanda cheo kutoka kuwa mhudumu wa mgahawani wa Kremlin.

Kikosi hicho kinaaminika kutumwa Ukraine tangu mwaka 2014, na tangu uvamizi wa Urusi mwezi Februari vikosi vya Ukraine vimefanya mashambulizi kwa kile wanachodai kuwa kambi za Wagner mashariki mwa Ukraine inayokaliwa kwa mabavu.

Mwezi Agosti, maafisa wa ulinzi wa Marekani walisema hadi wanajeshi 80,000 wa Urusi wameuawa au kujeruhiwa tangu vita vilipoanza mwezi Februari, na Moscow imeripotiwa kugeukia kundi la Wagner ili kuziba pengo lililoachwa na majeruhi hao wengi.

Mwezi uliopita, vyombo vya habari vya kujitegemea vya Urusi vilizungumza na wafungwa wanaozuiliwa katika vituo tofauti nchini Urusi ambao waliwaambia kwamba Bw Prigozhin alitembelea kituo chao kibinafsi ili kusajili wafungwa kujiunga na vita nchini Ukraine.