Rais Putin akusanya wanajeshi wa ziada kwa ajili ya vita Ukraine

Putin anasema nchi za Magharibi zimeonyesha kuwa hazitaki amani kati ya Ukraine na Urusi.

Muhtasari

•Rais wa Urusi Vladimir Putin ametangaza kukusanya wanajeshi wa ziada kwa ajili ya vita nchini Urusi.

•Putin pia anasema kuwa atatoa hadhi ya kisheria kwa ‘’wanaojitolea’’ wanaopigana huko Donbas

Putin ahutubia taifa
Image: Russian Presidential Press Service

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametangaza kukusanya wanajeshi wa ziada kwa ajili ya vita nchini Urusi - kulingana na shirika la habari linalomilikiwa na serikali TASS.

Anasema kuwa nchi za Magharibi zimeonyesha kuwa lengo lake ni kuiangamiza Urusi na kwamba zimejaribu kuwageuza watu wa Ukraine kuingia kwenye vita kwa lazima.

Lengo letu ni kuikomboa Donbas, anasema.

Rais Putin anasema nchi za Magharibi zimeonyesha kuwa hazitaki amani kati ya Ukraine na Urusi.

Putin pia anasema kuwa atatoa hadhi ya kisheria kwa ‘’wanaojitolea’’ wanaopigana huko Donbas.

Putin ametangaza kuwa kuanzia leo ni muhimu kuchukua uamuzi wa haraka ili kulinda watu katika ‘’ardhi zilizokombolewa’’.

“Ndiyo maana niliiomba wizara ya ulinzi kukusanya jeshi kwa ajili ya vita,” anasema.

Amesema agizo hilo tayari limetiwa saini na linaanza kutekelezwa leo.

Amesema kuwa raia wote ambao watakusnywa watakuwa na hadhi kamili ya jeshi.

Putin ameongeza kuwa nchi za Magharibi zimekuwa zikiichafua Urusi lakini Urusi ina silaha nyingi za kujibu.

“Tutatumia rasilimali zote tulizonazo kuwatetea watu wetu,” anasema.

‘’Nina imani na msaada wako,’’ anahitimisha.