Jumanne Novemba 15, 2022 dunia imeripotiwa kufikisha idadi ya watu bilioni 8 baada ya kuongezeka kwa zaidi ya watu bilioni moja kwa kipindi cha miaka 12 ambayo imepita.
Kulingana na utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu (UNFPA) India itaipiku China kwa idadi ya watu ifikapo mwisho wa 2023 .
UNFPA ilisema kuongezeka kwa idadi ya watu kwa kiwango cha juu ni ishara ya kuimarika kwa sekta ya afya duniani.
"Dunia yetu sasa ni nyumbani kwa watu bilioni 8 hivyo ni kumaanisha kuna Matumaini bilioni 8,ndoto bilioni 8 na majukumu bilioni 8" UNFPA iliandika kwenye Twitter.
Ripoti ya UNFPA inasema India inakadiriwa kuipita China kama nchi yenye watu wengi zaidi duniani mwaka wa 2023.
Ripoti ya matarajio ya idadi ya watu ilisema kwamba idadi ya watu nchini India itafikia bilioni 1.412 mwaka wa 2022, ikilinganishwa na Uchina yenye bilioni 1.426.
India inakadiriwa kuwa na idadi ya watu bilioni 1.668 mnamo 2050, mbele ya watu bilioni 1.317 wa Uchina kufikia katikati ya karne.