Uganda yawatoa hofu watalii kuhusu Ebola

"Uganda iko salama na wageni wa kimataifa wanakaribishwa," aliongeza.

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni
Image: BBC

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewahakikishia watalii kutoka mataifa ya kigeni kwamba mlipuko wa Ebola katika taifa hilo la Afrika Mashariki utadhibitiwa.

Katika hotuba yake kwa nchi siku ya Jumanne, rais Museveni alibainisha kuwa watalii wa kigeni walikuwa wakighairi kuweka nafasi na mikutano ya kimataifa ilikuwa inaghairishwa au kuhamishiwa katika nchi nyingine.

Alisema janga hilolipo ndani - na kesi zinazoendelea katika wilaya sita tu kati ya 146 kote nchini.

"Uganda iko salama na wageni wa kimataifa wanakaribishwa," aliongeza.

Alisema kuwa orodha ya watu walioambukizwa virusi hivyo imetolewa kwa mamlaka ya uhamiaji ili kuwazuia kusafiri kimataifa.

Baadhi ya kesi 141 zilizo na vifo 55 zimerekodiwa tangu kuzuka kwa ugonjwa huo kuthibitishwa mnamo Septemba.

Rais Museveni alisema kuwa mafanikio yamepatikana katika kudhibiti janga hilo. Kwa siku 18, hakukuwa na kesi zilizothibitishwa katika wilaya ya Mubende, kitovu cha mlipuko huo, ingawa kisa kimoja kiliripotiwa Jumatatu, kwa mujibu wa maafisa wa afya.

Bw Museveni alisema kuwa juhudi za kudhibiti janga hilo zinatatizwa na baadhi ya wananchi wanaokataa kuzingatia vikwazo vya afya. Usafiri wa pikipiki, unaojulikana kama boda boda, ulikuwa ukikaidi sheria za kutotoka nje katika maeneo yaliyoathiriwa na kusafirisha abiria badala ya mizigo pekee.

Katika wilaya ya Kassanda, watu 10 wa familia moja walikufa kwa ugonjwa wa Ebola baada ya kufukua maiti iliyozikwa na timu rasmi ya mazishi na kuzika tena kulingana na imani zao za kidini.

Jijini Kampala, watu wawili waliohusishwa na kesi tofauti walitoroka kutoka vituoni - moja hadi mji wa Masaka na mwingine katika jiji la Jinja - na wote wawili wamefariki dunia.

Ingawa janga hili limeenea katika wilaya mbali na kitovu katika eneo la kati, maafisa wa Uganda wanaonekana kuwa na imani kwamba mlipuko huo unaweza kudhibitiwa kabla haujasambaa.