Mashambulizi mapya yaiweka gizani miji ya Ukraine

Meya wa Lviv, Andriy Sadovy, alisema watoto wamepelekwa kwenye makazi na walimu wao

Muhtasari
  • Muda mfupi kabla ya ripoti mpya kutoka Kyiv na Lviv, maafisa walisema kusini mwa Ukraine kumekuwa na mashambulizi mapya

Mji wote wa magharibi mwa Ukraine wa Lviv hauna umeme, baada ya mashambulizi kuripotiwa kote Ukraine ikiwa ni pamoja na katika mji mkuu wa Kyiv.

Nchi jirani ya Moldova pia iliripoti kukatika kwa umeme, ingawa haijaathiriwa moja kwa moja.

Meya wa Lviv aliwataka watu kujilinda, wakati mkuu wa mkoa wa Kyiv alisema miundombinu muhimu na nyumba zimeshambuliwa. Urusi hivi karibuni imeongeza mashambulizi yake kwenye mitandao ya nishati ya Ukraine.

Hapo awali, tahadhari ya uvamizi wa anga ilitolewa kote Ukraine huku kukiwa na ripoti za milipuko katika maeneo kadhaa.

Meya wa Lviv, Andriy Sadovy, alisema watoto wamepelekwa kwenye makazi na walimu wao na akawataka wazazi wasiwachukue hadi kengele itakapoacha kulia.

Muda mfupi kabla ya ripoti mpya kutoka Kyiv na Lviv, maafisa walisema kusini mwa Ukraine kumekuwa na mashambulizi mapya.

Gavana wa eneo la Mykolaiv alionya kuhusu "roketi nyingi" zinazowasili kutoka kusini na mashariki. Katika eneo la karibu la Zaporizhzhia, mtoto mchanga aliuawa wakati kombora lilipopiga kitengo cha uzazi, huduma za dharura zilisema.