Waziri Namwamba amtembelea mtangazaji Catherine Kasavuli hospitalini na kumuombea (+picha)

Waziri pia alimuomba Kasavuli kuwa na kikao naye baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Muhtasari

•Kulingana na taarifa iliyotolewa na wizara ya Masuala ya Vijana, Michezo na Sanaa siku ya Jumapili, Namwamba alienda kumfariji mtangazaji huyo wa habari gwiji na kusali naye.

•Namwamba alisema kuwa ni heshima kuweza kumtembelea Kasavuli hospitalini na kusali naye.

Siku ya Jumamosi, waziri wa Masuala ya Vijana, Michezo na Sanaa Ababu Namwamba alimtembelea mwanahabari mkongwe aliyelazwa hospitalini, Catherine Kasavuli.

Kasavuli ,60, amekuwa akihudumiwa katika hospitali kuu ya Kenyatta kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja uliopita baada ya kugundulika na ugonjwa wa saratani ya shingo la uzazi.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na wizara ya Masuala ya Vijana, Michezo na Sanaa siku ya Jumapili, Namwamba alienda kumfariji mtangazaji huyo wa habari gwiji na kusali naye.

"Umetia moyo kizazi cha watangazaji wakuu wa kike. Ushawishi wako kwa wanahabari wetu wa kike hauwezi kulinganishwa kamwe. Mungu akupe uponyaji ili uendelee kuwashauri wasichana wetu,” Namwamba alisema wakati wa ziara ya hospitali.

Waziri pia alimuomba Kasavuli kuwa na kikao naye baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Kasavuli alianza kazi yake kama mtangazaji  wa mwendelezo wa redio katika Voice of Kenya (VOK) mwaka wa  1980 kabla ya kuhamia Televisheni. Hapo awali amewahi kufanya kazi katika KBC, Citizen na KTN News.

Huku akimtakia afueni ya haraka, Namwamba alisema kuwa ni heshima kuweza kumtembelea Kasavuli hospitalini na kusali naye.

Kasavuli alilazwa katika hospitali ya Kenyatta  mapema mwezi uliopita baada ya kugundulika na saratani ya shingo ya uzazi (Cervical Cancer).

Katika taarifa yake mwezi jana, alitoa shukran za dhati kwa familia yake, marafiki, wafanyikazi wenzake, Catherine Kasavuli Foundation, madaktari, wanamitandao na watu asiowajua ambao wamekuwa wa msaada mkubwa kwake.

"Natamani ningejibu meseji zenu zote, naziona na nashukuru sana. Mungu awakumbuke," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliongeza, "Kwa watu maalum ambao wamejitokeza kuchangia damu Mungu awabariki, azidishe roho zenu nzuri, atimize matakwa ya moyo wenu. Kwa wanaochangia bili yangu ya matibabu, ninawapenda sana na Mungu awabariki."

Kasavuli alidokeza kuwa vita vyake na ugonjwa wa saratani havijakuwa rahisi. Hata hivyo ameeleza imani yake kuwa hatimaye ataibuka mshindi. Pia amewatia moyo watu wengine wanaopambana na hali hiyo.

"Si safari rahisi lakini ninaamini katika uaminifu wa Mungu na mafanikio yake. Kwa mtu yeyote anayepigana vita sawa - nakupenda, tutashinda, maisha ni kitu kizuri na tutaishi kusimulia hadithi zetu," alisema.

Habari kuhusu kuugua kwa mtangazaji huyo wa KBC zilikuja kujulikana hadharani wiki jana ambapo ombi la damu lilitolewa kwa ajili yake. Taarifa fupi ilitolewa kuwa amelazwa katika KNH na watu wa kundi lolote la damu wakaombwa kujitolea.

"Wapendwa marafiki, wafanyakazi wenza na watu wenye nia njema. Mwenzetu mpendwa Catherine Kasavuli amelazwa katika Mrengo wa Kibinafsi wa KNH. Kwa wale wanaoweza, anahitaji kuwekwa damu mishipani haraka," taarifa iliyofikia Radio Jambo ilisoma.