Jeshi la Sudan lakubali kukabidhi madaraka

Maandamano ya kupinga makubaliano hayo tayari yameanza katika mji mkuu, Khartoum.

Muhtasari

•Mkataba huo unaruhusu kipindi cha mpito cha miaka miwili kinachoongozwa na raia kuelekea uchaguzi.

•Viongozi wa kisiasa wanasema wito wa haki na mageuzi mengine yatashughulikiwa kupitia mazungumzo zaidi.

Maelefu ya watu wakiandamana mjini Khartoum kuonyesha mshikamano wao na serikali ya mpito ya Sudan
Maelefu ya watu wakiandamana mjini Khartoum kuonyesha mshikamano wao na serikali ya mpito ya Sudan
Image: GETTY IMAGES

Muungano unaounga mkono demokrasia nchini Sudan wa Forces of Freedom and Change umetia saini makubaliano ya awali na jeshi kurejesha utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya mwaka jana.

Mkataba huo unaruhusu kipindi cha mpito cha miaka miwili kinachoongozwa na raia kuelekea uchaguzi.

Lakini maandamano ya kupinga makubaliano hayo tayari yameanza katika mji mkuu, Khartoum, na zaidi yanatarajiwa kote nchini, huku watu wakitaka walioongoza mapinduzi hayo kuwajibika.

Sudan imekumbwa na msukosuko wa kisiasa kwa takriban miaka minne baada ya aliyekuwa rais Omar al-Bashir kupinduliwa kufuatia maandamano makubwa.

Umoja wa Afrika, Mataifa ya Kiarabu na serikali za magharibi zimeunga mkono mazungumzo kati ya jeshi na raia kama njia ya kurejesha utulivu, kumaliza maandamano makubwa na kujaribu kuokoa uchumi unaoanguka wa Sudan.

Lakini makubaliano ya Jumatatu yanakabiliwa na upinzani mkali, haswa kutoka kwa kamati za upinzani za kitongoji ambazo zimekuwa kiini cha uhamasishaji wa mashinani.

Wanataka viongozi wa kijeshi akiwemo Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kuwajibika kwa vifo vya waandamanaji wanaopinga mapinduzi.

Mkataba huo pia hauangazii mageuzi ya sekta ya usalama na wengi wana wasiwasi kwamba unaacha jeshi likiwa na nguvu na kuweza kuvuruga mabadiliko ya kidemokrasia.

Viongozi wa kisiasa wanasema wito wa haki na mageuzi mengine yatashughulikiwa kupitia mazungumzo zaidi.