Askari watano ni miongoni mwa watu 26 waliouawa katika shambulio Somalia

Milio ya risasi na milipuko ilisikika mapema Jumanne wakati jeshi likipambana na wanamgambo hao.

Muhtasari
  • Waliofariki ni pamoja na wanajeshi watano wa kitaifa na wapiganaji 21 wa kundi la wanamgambo wa al-Shabab
Image: BBC

Mamlaka ya nchini Somalia zimesema watu 26 wameuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulio la Jumanne asubuhi kwenye kambi ya kijeshi katika mji wa Hawadley, katika eneo la Shabelle ya Kati.

Waliofariki ni pamoja na wanajeshi watano wa kitaifa na wapiganaji 21 wa kundi la wanamgambo wa al-Shabab.

Shambulizi hilo lilianza baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kuvamia kituo hicho.

Milio ya risasi na milipuko ilisikika mapema Jumanne wakati jeshi likipambana na wanamgambo hao.

Shambulio hilo linakuja siku chache baada ya jeshi kuteka bandari ya kimkakati ya Haradhere, ambayo imekuwa ikishikiliwa na kundi la al-Shabab kwa miaka 15.

Al-Shabab wamepoteza maeneo mengi tangu Agosti mwaka jana, wakati wanajeshi wa serikali wakisaidiwa na wanamgambo wa koo walipoanzisha mashambulizi kusini na katikati mwa Somalia.

Lakini kundi hilo limeendelea kufanya mashambulizi yanayolenga hasa majengo ya serikali na wanajeshi wa Umoja wa Afrika.

Wiki iliyopita, ilifanya mashambulizi manne mabaya ya mabomu katika eneo la kati la Hiram.