Wanamgambo wawatia viboko na mijeledi wanawake kwa kuvaa sketi fupi, suruali

Wanamgambo hao walidai hatua hiyo ni kuhimiza adhabu kali za Sharia za Kiislamu katika eneo ambalo wanadhibiti.

Muhtasari

• Waziri mkuu wa DRC alisema wanamgambo hao watachukuliwa hatua kali kwa kuwadhulumu wanawake.

Mwanamke mwenye sketi fupi
Mwanamke mwenye sketi fupi
Image: MPASHO NEWS

Wanawake na wasichana nchini Jahmhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walichapwa viboko na mijeledi mikali na wanamgambo mashariki mwa taifa hilo lenye vikundi vingi vya wanamgambo kwa kuvaa sketi fupi na suruali.

Kulingana na AFP, waziri mkuu Jean Michele Sama Lukonde alitoa taarifa hiyo Jumamosi na kusema kuwa wanamgambo hao wataadhibiwa vikali kwa kuwanyanyasa wanawake na wasichana.

 Waziri Mkuu Jean-Michel Sama Lukonde "alilaani unyanyasaji wa udhalilishaji na unyama unaofanywa na wanamgambo" kutoka kundi la Malaika lenye silaha, kulingana na usomaji wa mkutano wa baraza la mawaziri uliochapishwa Jumamosi.

Lukonde alisema wanamgambo hao ambao wanatoa adhabu za sharia za Kiislamu katika eneo ambalo wanadhibiti, hivi karibuni "wamewachapa viboko wasichana na wanawake waliovalia sketi fupi na suruali".

Ujumbe wa serikali utatumwa katika eneo hilo -- Salambila, katika jimbo la mashariki la Maniema -- na kuripoti ili wahusika waadhibiwe, Lukonde alisema.

Wanamgambo wa Malaika, ambao wanadai kuwakilisha maslahi ya wenyeji, wanataka serikali kukabidhi sehemu kubwa ya mapato kutoka migodi ya dhahabu ya Salamabila.

Ni moja ya makundi kadhaa yenye silaha ambayo yanafanya kazi kwa uhuru katika eneo lenye hali tete, lenye utajiri wa madini mashariki mwa nchi hiyo kubwa ya Afrika ya Kati.

Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mbalimbali na eneo hilo kwa muda limekumbwa na mizozo ya vita baina ya serikali na makundi ya wanamgambo wenye silaha ambao wanadai kudhibiti eneo hilo.

Kundi la Malaika linadai kuwakilisha maslahi ya Kiislamu na ni mojawapo na vikundi vyenye silaha vinavyowahangaisha watu wa eno hilo, haswa Wakristu.

Haya yanajiri wakati ambapo taifa hilo jipya kujiunga na ukanda wa Afrika Mashariki likiendelea na mazungumzo ya Amani baina ya serikali na wanamgambo wa kundi hatari la M23.

Mazungumzo ya Amani yamekuwa yakiongozwa na rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta ambapo taarifa zinadai mazungumzo hayo yamefikia hatua muhimu za kuweka silaha kando ili kudumisha Amani.