Mwalimu ashambuliwa na nyuki hadi kufa papo hapo!

Si mara ya kwanza kwa nyuki hao kufanya madhara, mara ya kwanza waliwahi shambulia mifugo na mbwa wawili walikufa.

Muhtasari

• Nyuki walikuwa wengi na juhudi za majirani kumuokoa mwalimu huyo ziligonga mbwamba.

• Wanakijiji walitaka mamlaka za maliasili kufanya mchakato wa haraka na kuwaondoa nyuki hao na ikiwezekana mwembe kukatwa.

Nyuki
Nyuki
Image: University of Melbourne

Mwalimu mmoja katika mkoa wa Kigoma nchini Tanzania ameripotiwa kufariki papo hapo baada ya kushambuliwa na nyuki.

Deogratius Emili Ndokoye mweney umri wa miaka 51 alikuwa mwalimu katika shule ya msingi ya Mambo iliyopo manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kulingana na taarifa zilizoripotiwa na Ayo TV, nyuki hao walikuwa kwenye mti wa mwembe nyumbani kwa mwalimu huyo wakati watoto waliokuwa wakicheza walirusha mawe na kuamsha ghadhabu yao.

Nyuki walitoka kwa fujo kumtafuja aliyewachokoza na kumshambulia mwalimu huyo huku watoto wakiwa wamechana mbuga.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Masanga, Lubabi Aron Nyabakali aliambia Ayo TV tukio hilo sio la kwanza katika eneo hilo, mara ya kwanza nyuki hao walivamia mifugo ambapo mbwa wawili walikufa na kuziomba Mamlaka za Maliasili kufanya harakati za kuwatoa nyuki hao na ikibidi mwembe huo ukatwe kwa ajili ya usalama wa wananchi.

 

Majirani walisema walifanya jitihada za kuyaokoa maisha yake lakini hawakufanikiwa kwa kuwa nyuki walikuwa wengi na wakashindwa namna ya kuwadhibiti kwa uharaka zaidi.

 

Marehemu mwalimu Deogratius amecha Mke na Watoto watatu, mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao Nyabitaka tarafa ya Mabamba iliyopo Wilayani Kibondo kwaajili ya hatua nyingine za mazishi, blogu hiyo iliripoti.