Mkuu wa mamluki wa Urusi Yevgeny Prigozhin ameweka picha ya wanajeshi wake waliofariki nchini Ukraine mtandaoni, akilaumu wakuu wa jeshi kwa vifo hivyo na kutaka Warusi wa kawaida kusaidia kundi lake.
Prigozhin alikuwa tayari ameanza vurugu siku ya Jumanne, akimshutumu waziri wa ulinzi na mkuu wa majeshi kwa kujaribu kumaliza mamluki wake wa Wagner kwa kuwanyima silaha.
Mamluki wa Wagner wamehusika sana katika kuzingirwa kwa eneo la Bakhmut mashariki mwa Ukraine.
Hata hivyo wizara ya ulinzi ilikanusha madai yake.
"Taarifa zote zinazodaiwa kutekelezwa na vitengo vya uvamizi juu ya uhaba wa silaha sio kweli kabisa," ilisema, bila kutaja jina Prigozhin au kikundi cha Wagner.
Ikielezea kupeana silaha kwa vikundi vya mamluki kama kipaumbele, wizara iliorodhesha roketi 1,660, mizinga na mota 10,171 na vifaru 980 ilikuwa vimetolewa kati ya Jumamosi 18 Februari na Jumatatu iliyofuata.
Prigozhin, ambaye alianzisha kundi la Wagner, kwa miaka mingi alikuwa na uhusiano wa karibu na Rais wa Urusi Vladimir Putin lakini vita vya Ukraine vimesababisha ushindani mkali kati ya mamluki na jeshi la kawaida, na wachambuzi wanaamini kuwa hasikilizwi tena na rais.
Makundi ya mamluki kama vile Wagner yanadaiwa kuwa haramu nchini Urusi lakini Prigozhin hajalisajili tu kama kampuni lakini pia ilirekodiwa mwaka jana ikisajili waziwazi makurutu kwa ajili ya vita kutoka kwa magereza ya Urusi.
Mwezi uliopita Wagner ilidai ushindi katika mji wa mashariki wa Soledar, lakini wizara ya ulinzi ikasema baadaye kwamba ilikuwa inaudhibiti mji huo.
Mapigano eneo la Bakhmut yameendelea kwa zaidi ya miezi sita na limekuwa mlengwa mkuu katika mashambulizi ya Urusi upande wa mashariki.
Kampeni hiyo inaaminika kugharimu maelfu ya maisha.
Akishindwa kujizuia, Prigozhin alilalamika kwamba Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu na Mkuu wa Wafanyikazi, Valery Gerasimov hawakuzuia tu silaha kutumwa lakini hawakusaidia na usafiri wa anga au hata kutoa koleo kwa ajili ya kuchimba mitaro.
Upinzani kama huo wa moja kwa moja ndani ya jeshi wa kuwapa wapiganaji wake vifaa ulifikia hatua ya uhaini, alisema.
Wizara ilipokanusha madai yake, alijibu akielezea kauli yake kama "kumtemea mate" Wagner, akilalamika kuwa halikupokea asilimia 80 ya silaha walizoomba ili kutekeleza misheni yao ya mapigano.
Kisha aliweka picha, inaonekana kutoka eneo la Bakhmut, ya maiti za makumi ya mamluki waliouawa kwenye vita zikiwa zimelala kwenye ardhi iliyoganda zikisubiri kukusanywa.
"Hawa ndio watu waliokufa jana kwa sababu ya kile kinachoitwa 'upungufu wa silaha'. Ni mara tano zaidi kuliko inavyopaswa kuwa," alisema katika ujumbe wa sauti kwa huduma yake ya vyombo vya habari.
Alitoa wito kwa Warusi kudai hadharani, lakini bila kutumia maandamano, kwamba wizara ya ulinzi itoe risasi kwa wanajeshi wake.
Mgogoro wa madaraka katikati ya vita vya Urusi nchini Ukraine umewafanya wachambuzi kutafakari iwapo Prigozhin anaondolewa na Jenerali Gerasimov, ambaye hivi karibuni aliwekwa kuwa msimamizi wa kampeni hiyo.
Mchambuzi anayeiunga mkono Kremlin Sergei Markov alisema Warusi waliounga mkono vita hivyo ni wazi wanamuunga mkono Prigozhin na ugomvi huo utadhoofisha mamlaka ya wizara ya ulinzi.
Mtaalamu wa Urusi Mark Galeotti alisema kwamba ikiwa silaha zilikuwa zinazuiliwa wakati huo, pamoja na uhuru wa mamluki wa Wagner kubanwa huko Bakhmut, "inaweka mazingira kwa watu wa kawaida kumpa Putin ushindi wake wa kwanza (ingawalitakosa maana) kwa kiasi fulani".
"Hatutaondoka Bakhmut," aliapa Prigozhin katika ujumbe wake wa sauti. "Tutakufa kwa idadi maradufu hadi wote [Wagner] wamalizike. Na Wagner watakapokamilika, kuna uwezekano mkubwa Shoigu na Gerasimov watalazimika kuchukua mtutu wa bunduki."