Kwa nini wanawake wa China hawataki kupata watoto

Gharama ya juu ya kulea mtoto pia ni sababu inayochangia wanawake kutotaka watoto.

Muhtasari

• China inakabiliwa na mabadiliko ya idadi ya watu: idadi ya watu inapungua kwa mara ya kwanza katika miongo sita.

Image: GETTY IMAGES

"Siwezi kumudu watoto," anasema Gloria ambaye ameolewa na katika miaka yake ya 30.

Amepiga hesabu na kubaini kwamba ingemgharimu karibu dola 2,400 kwa mwezi juu ya matumizi yake mengine ya kulea mtoto anakoishi nchini China.

"Itakuwa yuan 3,000 ($436) kwa matumizi ya kila siku kama vile chakula. 2,000 ($291) kwa shule ya chekechea, 1,000 ($145) kwa ajili ya malezi ya muda ya watoto ikihitajika na angalau 10,000 ($1,456) kwa ajili ya shule."

Gloria anafanya kazi kwa muda kama mwalimu wa shule ya msingi katika mkoa wa Guangdong kusini mwa China.

Wastani wa mapato kwa wale wanaofanya kazi katika sekta ya kibinafsi katika sehemu hii ya nchi ni takriban yuan 6,000 kwa mwezi ($873).

Akiwa mtoto pekee katika familia yake, kutokana na sera ya Uchina ya kuwa na mtoto mmoja, anasema anahitaji kuzingatia kulipa mkopo wake wa nyumba na kuwawekea akiba wazazi wake wanaozeeka.

Idadi ya watu inayopungua

China inakabiliwa na mabadiliko ya idadi ya watu: idadi ya watu inapungua kwa mara ya kwanza katika miongo sita.

Na data mpya inaonyesha wanawake wengi wa China wanataka mtoto mmoja tu au hawataki kabisa mtoto.

Asilimia ya wanawake wa China ambao hawakuwa na watoto ilipanda kutoka 6% mwaka 2015 hadi 10% mwaka 2020, kulingana na utafiti wa hivi karibuni wa Kituo cha Utafiti wa Idadi ya Watu na Maendeleo ya China.

Pia ilionyesha wanawake wa China walio katika umri wa kuzaa wana nia ya chini ya uzazi, na wastani wa idadi inayotarajiwa ya watoto imeshuka hadi 1.64 mwaka 2021 ikilinganishwa na 1.76 mwaka 2017.

Ingawa nchi nyingine za Asia kama Singapore, Japan na Korea Kusini pia zina kiwango cha uzazi chini ya mbili, baadhi ya watu wanasema bado wanatarajia kupata watoto wawili. Huko China, sio hivyo.

"Kwa maana hii, Uchina ni ya nje kwa sababu sio tu kwamba uzazi halisi uko chini, lakini hamu ya uzazi pia iko chini," anasema Dk Shuang Chen, profesa msaidizi katika Sera ya Kimataifa ya Jamii na Umma katika chuo cha masuala ya Uchumi na Sayansi ya Siasa cha London.

China inapoanzisha mikutano yake ya kisiasa ya "vikao viwili" - muhimu zaidi mwaka - tarehe 4 Machi, washauri wa kisiasa wamewasilisha mapendekezo mbalimbali juu ya kuongeza kiwango cha uzazi.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kusaidia wanawake ambao hawajaolewa kugandisha mayai na kuondoa ada ya masomo na vitabu vya kiada kutoka shule ya chekechea hadi chuo kikuu.

Wazo lingine ni kuwapa watoto waliozaliwa na wazazi ambao hawajaoana haki sawa.

Nchini China, watoto wanaozaliwa na wazazi ambao hawajaoa wana matatizo ya kupata "hukou", usajili rasmi wa kijamii unaohitajika kwa ajili ya elimu, huduma za afya na ustawi wa kijamii, na ada za usimamizi zinaweza kuwa ghali.

Gharama ya juu ya kulea mtoto

Image: GETTY IMAGES

Gharama ya juu ya kulea mtoto ni mojawapo ya sababu kuu za wanawake wa China kutotaka kujifungua.

"Sitaki kuanza maisha mapya katika mazingira ya ushindani wa hali ya juu," anasema Mia, mwanafunzi wa chuo mwenye umri wa miaka 22 .

Alizaliwa katika mji mdogo kaskazini mwa Uchina, Mia alipata elimu yake ikizingatia mitihani. Alifanya mtihani wa kuingia chuo kikuu cha kitaifa cha China, unaojulikana kama Gaokao, na baadaye akajiunga na chuo kikuu cha kifahari huko Beijing.

Lakini anasema mara nyingi alihisi kukumbwa na msongo wa mawazo.

Wahitimu leo, anabainisha, lazima pia washindane na wale ambao wamepata njia za kusoma nje ya nchi.

"Msaada huu wote wa ziada wa elimu unahitaji pesa," anasema Mia, ambaye hafikirii kuwa anaweza kupata pesa za kutosha kwa watoto wajao kupewa fursa kama hizo.

"Ikiwa siwezi kumpa mtoto kustawi kwa njia hii, basi kwa nini nimlete katika ulimwengu huu?"

Uwiano wa maisha na kazi

Wanawake wengi wana wasiwasi kwamba kupata watoto kunaweza kuathiri vibaya kazi zao.
Wanawake wengi wana wasiwasi kwamba kupata watoto kunaweza kuathiri vibaya kazi zao.
Image: GETTY IMAGES

Wanawake wa BBC Idhaa ya Kichina waliohojiwa pia walitaja athari mbaya katika taaluma zao kuwa sababu iliyowafanya kuchagua kutokuwa na watoto.

Katika mahojiano ya kazi, wanawake hao walikumbuka kuwa wangeulizwa ikiwa walipanga kupata watoto katika miaka michache ijayo. Wanasema kwamba ikiwa walijibu ndiyo, basi uwezekano wa wao kuajiriwa ulikuwa mdogo, au wangekuwa na nafasi ndogo ya kupandishwa cheo.

"Uwiano wa maisha na kazi ni jambo linalosisitizwa sana na wanawake wa China katika elimu ya juu wakati wanazingatia kama wako tayari kupata mtoto," Dk Yun Zhou, profesa msaidizi wa sosholojia katika Chuo Kikuu cha Michigan, aliiambia. BBC.

"Kazi kwao ni kujitambua," alisema. "Katika soko la ajira lililosheheni ubaguzi wa kijinsia, ni vigumu kuchagua kati ya kazi na kuwa na mtoto."

'Nilinyanyaswaje mtandaoni baada ya kusema sitaki kuzaa'

Kama vijana wengi ambao wanapenda kushiriki maisha yao kwenye mitandao ya kijamii, Mia alirekodi video akieleza kwa nini alitaka kubaki bila mtoto na akaichapisha kwenye mtandao.

Kwa mshangao wake, alipokea mamia ya maoni ya matusi.

Wengi walimshutumu kuwa mbinafsi. Wengine walisema hakujua akili yake mwenyewe kwani bado alikuwa na umri wa miaka 20.

"Huna kile kinachohitajika kusema hivyo. Angalia ikiwa bado unafikiri hivyo unapokuwa katika miaka ya 40," mtumiaji mmoja alitoa maoni.

"Nina weka dau la dola 10,000 utajuta," mwingine alisoma.

Wengine wamefikia hatua ya kumwita “jeshi la kigeni” ambalo “linawachochea” watu wasizae.

Serikali ya China ilianzisha sera yake ya watoto watatu mwezi Mei 2021 kujibu matokeo ya sensa ya 2020, ambayo yanaonyesha akina mama wa China walijifungua watoto milioni 12 tu mwaka huo, idadi ndogo zaidi ya watoto waliozaliwa tangu 1961.

Serikali katika miaka ya hivi karibuni imeanzisha sera nyingi mpya za kuhimiza watu wengi zaidi kupata watoto.

Lakini kutokana na viwango vya chini vya uzazi vya Uchina, kwa macho ya baadhi ya wanawake, mwanamke ambaye hataki kuzaa anaiangusha nchi hiyo.

"Ni chaguo langu binafsi. Sitetei wazo la kutozaliwa. Ninaheshimu watu wanaotaka watoto," Mia anasema.