Matiang'i awasili katika makao makuu ya DCI

Matiang'i anasakwa kuhojiwa kuhusiana na madai ya polisi kuvamia nyumba yake.

Muhtasari

• Matiang'i alikuwa ameandamana na mawakili wake wakiongozwa na Danstan Omari, aliyekuwa waziri Eugene Wamalwa, seneta wa Kisii Richard Onyonka miongoi mwa viongozi wengine wengi. 

Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i tayari amewasili katika makao makuu ya DCI.

Mawakili wa Matyang’i walikuwa wamesema kwamba mteja wao angewasili katika makao makuu ya DCI mwendo wa saa mbili, saa moja kabla ya muda aliyoelekezwa.

Wakili wake Danstan Omari alisema kwamba alimwandikia afisa wa mwaliko kumjulisha kuhusu mabadiliko hayo.

"Tunathibitisha kuwa tutakuwepo, hakuna chochote cha kuficha," alisema.

Matiang'i anasakwa kuhojiwa kuhusiana na madai ya polisi kuvamia nyumba yake huko Karen usiku wa Februari 8.

Polisi na idara zote za usalama walikanusha kuhusika na uvamizi huo wakidai kuwa uzushi.

Omari alisema waziri huyo wa zamani yuko tayari kurekodi taarifa yake kuhusu uvamizi huo akisema hangeweza kufanya hivyo hapo awali kwa vile wito uliotolewa Februari 23 hawakupewa kamwe.

"Hatujawahi kwenda huko kwa sababu hatujawahi kupewa mwaliko rasmi. Nimepokea leo, tukathibitisha kuwa sisi ni raia wanaotii sheria. Tutampeleka CS huko kesho," Omari alisema.