Shambulio baya la risasi lafanyika katika Jumba la Jehovah Witness Ujerumani

Watu kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi kwenye jumba la mikutano la Jehovah Witness mjini Hamburg.

Muhtasari

• Polisi wanasema walimpata mtu aliyekufa katika eneo la tukio ambaye wanaamini kuwa huenda alikuwa mhusika na uchunguzi unaendelea.

Maafisa wa polisi wakikabiliana na mshukiwa huko Ujerumani
Maafisa wa polisi wakikabiliana na mshukiwa huko Ujerumani
Image: BBC

Watu kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi kwenye jumba la mikutano la Jehovah Witness katika jiji la Hamburg kaskazini mwa Ujerumani.

Polisi wanasema kuwa mtu aliyepiga risasi alikuwa pekee na anadhaniwa amekufa. Haijabainika iwapo mshambuliaji huyo ni miongoni mwa vifo sita au saba vilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya Ujerumani.

Bado, "hakuna taarifa za kuaminika juu ya nia yake," polisi wanasema.

Watu kadhaa pia walijeruhiwa katika ufyatulianaji wa risasi kwenye mtaa wa Deelböge katika wilaya ya Gross Borstel ya jiji hilo.

Polisi wanasema walimpata mtu aliyekufa katika eneo la tukio ambaye wanaamini kuwa huenda alikuwa mhusika na uchunguzi unaendelea.

Polisi waliitwa mwendo wa 21:15 (20:15 GMT) kufuatia ripoti kwamba kuripoti kwamba risasi zilifyatuliwa kwenye jengo hilo, msemaji wa polisi Holger Vehren alisema.

Maafisa walioingia ndani walipata watu ambao "huenda wamejeruhiwa vibaya na risasi, baadhi yao wakiwa wamepoteza maisha", alisema.

"Maafisa hao pia walisikia mlio wa risasi kutoka sehemu ya juu ya jengo hilo na wakapanda juu, ambapo pia walimkuta mtu. Hadi sasa hatuna dalili zozote kwamba wahalifu wowote walitoroka."

Alisema polisi bado hawajawatambua wahasiriwa na uchunguzi katika eneo la uhalifu inaendelea.