Watu 8 wafa maji wakichimba dhahabu magharibi mwa Tanzania

Wanane hao walikufa baada ya shimo kujaa maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika mkoa wa Geita.

Muhtasari

•Aidha mmoja alinusurika huku vikosi vya uokoaji vikifanikiwa kuopoa miili nane kutoka kwenye shimo hilo jana.

•Kazi ya uokoaji ilifungwa jana ambapo walipata miili nane na mtu mmoja alitoka akiwa hai.

crime scene
crime scene

Wachimbaji wadogo nane wamepoteza maisha Magharibi mwa Tanzania baada ya shimo waliloingia kuchimba dhahabu kujaa maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika mkoa wa Geita.

Aidha mmoja alinusurika huku vikosi vya uokoaji vikifanikiwa kuopoa miili nane kutoka kwenye shimo hilo jana.

Mamlaka zinasema wachimbaji hao waliingia kinyume cha sheria kutafuta dhahabu katika handaki lisilokuwa salama ambalo lilikuwa na leseni ya shughuli za utafiti pekee.

Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Safia Jongo aliiambia BBC kuwa kazi ya uokoaji ilifungwa jana ambapo walipata miili nane na mtu mmoja alitoka akiwa hai.

"Walichokifanya ni kuhatarisha maisha yao, na watu wengi, haswa vijana huchukua hatari kama hizi kwa kuingia maeneo hatarishi bila kujali athari...

"...huwa tunawasihi wasiingie kwenye mashimo ikiwa hawana leseni ya shughuli hiyo. Tahadhari za usalama huwekwa wakati mtu ana leseni ya kufanya kazi, vinginevyo unapovamia unakuwa katika hatari kubwa," alisema kamanda huyo.

Kamanda huyo pia amewaonya wachimbaji ambao wamekuwa wakivamia mashimo yenye miliki kuacha kwa sababu ni kinyume na sheria.

Geita ni miongoni mwa maeneo yanayoripotiwa kuwa na akiba kubwa ya dhahabu katika upande wa magharibi mwa Tanzania