Mwanamume ashambuliwa na tembo aliyetoroka hifadhi wakati anajipiga ‘selfie’ naye

Ni sehemu ya kundi la wanyama waliotoroka eneo la hifadhi katika mkoa wa Manyara kaskazini

Muhtasari
  • Kamishna wa polisi wa eneo hilo alisema tembo hao walikasirika na kuanza kuchanganyikiwa baada ya kundi la wenyeji kuwakaribia na kuanza kupiga selfie nao.

Mwanaume mmoja raia wa Tanzania yuko katika hali mbaya hospitalini baada ya kujipiga picha yaani ‘selfie’ na tembo yaani ndovu kabla ya kumgeukia na kumshambulia.

Ni sehemu ya kundi la wanyama waliotoroka eneo la hifadhi katika mkoa wa Manyara kaskazini na kula mazao ya shambani katika kijiji kimoja, kwa mujibu wa mamlaka.

Kamishna wa polisi wa eneo hilo alisema tembo hao walikasirika na kuanza kuchanganyikiwa baada ya kundi la wenyeji kuwakaribia na kuanza kupiga selfie nao.

“Mtu huyo amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Kiteto na anaendelea na matibabu...hali yake imeimarika kidogo,” alisema George Katabazi.

Migogoro kati ya binadamu na wanyamapori ni jambo la kawaida nchini Tanzania, ambapo vipindi vya ukame mara nyingi husababisha wanyamapori kukimbilia mashambani kutafuta chakula.