logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mapenzi ya jinsia moja yanalazimishwa kwetu na nchi za Magharibi - Museveni

“Tunahitaji kuuliza swali; 'ni kwa asili au kwa malezi'," Bw. Museveni aliongeza.

image
na Radio Jambo

Burudani16 March 2023 - 15:55

Muhtasari


  • Wanaharakati wa LGBTQ wanasema jumuiya yao imekabiliwa na unyanyasaji wa kimwili na mtandaoni katika wiki za hivi karibuni.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa nchi za Magharibi hazipaswi kulazimisha desturi zao kwa Waafrika kwa kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja.

Katika hotuba yake maalum kwa Bunge siku ya Alhamisi, rais aliongeza kuwa mapenzi ya jinsi moja ni kupotoka au kuondokana na kile kilicho cha kawaida.

“Tunahitaji kuuliza swali; 'ni kwa asili au kwa malezi'," Bw. Museveni aliongeza.

"Kufanya mapenzi nchini Uganda na maeneo mengine ya Afrika ni siri. Hata kwa wapenzi wa jinsia tofauti. Tutajuaje kuwa wewe unashiriki mapenzi ya jinsia moja, labda utangaze?” Aliendelea kusema.

Maoni yake yanakuja wakati ambapo kuna wimbi la chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja linaloenea kote nchini humo na ukanda wa Afrika mashariki.

Wanaharakati wa LGBTQ wanasema jumuiya yao imekabiliwa na unyanyasaji wa kimwili na mtandaoni katika wiki za hivi karibuni.

Mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja uliwasilishwa katika bunge la Uganda mapema mwezi huu.

Unatafuta kuifanya kuwa haramu kwa mtu yeyote kujitambulisha kama anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Pia unaagiza kifungo cha miaka kumi jela kwa kujihusisha na mahusiano au ndoa ya jinsia moja, pamoja na kukuza shughuli zinazohusiana na mapenzi ya jinsia moja au uanaharakati.

Mswada huo kwa sasa unachunguzwa na kamati ya bunge kuhusu masuala ya sheria.

Prof. Sylvia Tamale, msomi mashuhuri ambaye alifika mbele ya kamati siku ya Alhamisi ili kushirikisha maoni yake, alikosoa sheria iliyopendekezwa kwa "kujaribu kupoteza kabisa utambulisho wa sehemu ya jamii" na kwa kuchanganya uhalifu kama vile kulawiti watoto na mapenzi ya jinsia moja.

Sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja, ambayo imeweka adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kosa hilo, ilibatilishwa na mahakama ya kikatiba mwaka 2014 kwa msingi kwamba ilipitishwa bila kuwepo kwa idadi ya wabunge inayotakiwa bungeni.

 

 

 

 


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved