Sudan Kusini:Wanahabari waliohusishwa na video ya rais akitokwa na haja ndogo wachiliwa huru

Kukamatwa huko kumeshutumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu

Muhtasari

•UJOSS imesema katika taarifa yake kwamba unafurahishwa na kuachiliwa kwa Victor Ladu na Mustapha Osman.

•Wafanyikazi sita kutoka shirika la utangazaji la serikali walikamatwa baadaye, lakini wawili bado wanazuiliwa.

Image: BBC

Wanahabari wawili kati ya wanne waliozuiliwa mwezi Januari baada ya video inayomuonyesha rais wa Sudan Kusini akilowesha suruali yake kwenye hafla ya hadhara wameachiliwa.

Muungano wa chama cha Wanahabari Sudan Kusini (UJOSS) umesema katika taarifa yake kwamba unafurahishwa na kuachiliwa kwa Victor Ladu na Mustapha Osman.

Mnamo mwezi Desemba mwaka jana, video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilionekana kumuonyesha Bw Kiir akijikojolea huku wimbo wa taifa ukipigwa kwenye hafla.

Wafanyikazi sita kutoka shirika la utangazaji la serikali walikamatwa baadaye, lakini wawili bado wanazuiliwa.

"[Tunaitaka] serikali kuwaachilia huru Garang John na Jacob Benjamin au ikiwa wana kesi ya kujibu, wanapaswa kuwasilishwa katika mahakama ya sheria," taarifa ya UJOSS ilisema.

Kukamatwa huko kumeshutumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ikiwa ni pamoja na Kamati ya Kulinda Wanahabari (CPJ).

Kukamatwa kwa watu hao kunalingana na "mtindo wa maafisa wa usalama kuzuia wat kiholela wakati maafisa wanaona kuwa utangazaji wao haufai", alisema mwakilishi wa CPJ Kusini mwa Jangwa la Sahara, Muthoki Mumo alisema wakati huo.