Mwanafunzi aangukiwa na jiwe kichwani ka kufa akifanya adhabu ya mwalimu shuleni

Inaarifiwa mwanafunzi huyo (msichana) wa kidato cha kwanza alipewa adhabu ya kuchimba kifusi baada ya kukutwa akizungumza Kiswahili badala ya Kiingereza.

Muhtasari

• Mwanafunzi huyo wa kike aliangukiwa na jiwe kubwa kwenda ndani ya shimo alimokuwa akichimba kama adhabu ya mwalimu mkuu.

•Jiwe hilo lilimuangukia kichwani na kumpasua kifua hadi utumbo ukatoka nje, kifo ambacho kilitajwa kama cha ukatili.

Mwanafunzi wa kike aangukiwa na jiwe kichwani akichimba shimo kama adhabu ya mwalimu mkuu
Mwanafunzi wa kike aangukiwa na jiwe kichwani akichimba shimo kama adhabu ya mwalimu mkuu
Image: Screengrab

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwanafunzi wa shule ya upili nchini Tanzania ameripotiwa kufariki baada ya kuangukiwa na jiwe kichwani.

Mwanafunzi huyo anasemekana kupatwa na mwalimu mkuu akizungumza Kiswahili badala ya Kiingereza na kukabidhiwa adhabu ya kuchimba vifusi katika sehemu iliyokuwa na mawe makubwa.

Akiwa shimoni kuchimba, jiwe moja liliporomoka na kumuangukia kichwani na kumuua papo hapo katika kile mashuhuda walisema ni kifo cha ukatili.

Jiwe hilo kubwa lililoporomoka pia liliwajeruhi wanafunzi sita huku mmoja wao akivunjika mguu wa kulia na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Kulingana na mzazi mmoja aliyekuwa akilalama, wanafunzi katika shule za msingi nchini Tanzania huwa hawafunziw Kiingereza na huyo ndio mara ya kwanza alikuwa amejiunga kidato cha kwanza akitokea msingi.

“Mwalimu mkuu ni mwanamke na watoto walikutwa wanaongea Kiswahili wakapewa adhabu ya kuchimba kifusi. Mmoja aliyekuwa ndani aliangukiwa na jiwe kubwa likampasua kichwa, likampasua utumbo wote ukawa nje, amekufa pale pale kifo cha ukatili kabisa,” mzazi huyo alieleza kwa uchungu.

Inaarifiwa kwamba mwalimu huyo mkuu mtoa adhabu baada ya kutaarifiwa kuhusu kilichotokea, alikimbia kwa kutumia pikipiki huku akiacha kila kitu chake nyuma ikiwemo leso na vitabu.

Kamanda wa polisi alidhibitisha kisa hicho na kusema kwamba wanafunzi hao ni miongoni mwa 30 waliopewa adhabu hiyo kali na isiyofaa kwa watoto wadogo.

“Wanafunzi ambao walikuwa wameongea lugha ya Kiswahili katika mazingira ya shule. Watoto Zaidi ya 30 na adhabu yenyewe ilikuwa ni kuchimba kifusi ili kuchota mchanga wa kuziba mtaro wa kupitisha maji. Mwanafunzi wa kike ndiye alifariki,” kamanda wa polisi alisema.