Bunge la Uganda lapitisha tena muswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja

Muswada huo ulipitishwa kwa wingi wa kura. Ni mbunge mmoja tu aliyepinga.

Muhtasari

• Muswada huo umelaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu.

Image: REUTERS

Bunge nchini Uganda, kwa mara ya pili, limepitisha mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja unaotoa adhabu ya kifo kwa kile kinachojulikana kama makosa ya kukithiri. Mswada huo uliopitishwa kwa mara ya kwanza mwezi Machi, ulirejeshwa bungeni na mapendekezo kutoka kwa Rais Yoweri Museveni kwamba marekebisho yafanywe.

Kifungu ambacho kilihalalisha watu kwa kujitambulisha tu kama LGBTQ+ kimerekebishwa.

Rais Museveni alisema kuwa kifungu hicho kingesababisha kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa watu kwa sababu ya sura zao tu, hata kama hawajafanya uhalifu wowote kama ilivyoainishwa na mswada huo.

Hii ina maana kwamba uhalifu wa mapenzi ya jinsia moja chini ya sheria inayopendekezwa utahusu tu vitendo vya ngono kati ya watu wa jinsia moja. Watu waliopatikana na hatia chini ya kifungu hiki wanakabiliwa na kifungo cha maisha.

Chini ya sheria inayopendekezwa, umma utalazimika kuripoti kwa mamlaka, aina yoyote ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto au watu wengine walio katika mazingira magumu unaofanywa na wapenzi wa jinsia moja katika jamii yao.

Wamiliki wa nyumba wanaokodisha kwa kujua majengo ambayo hutumiwa kwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja wanaweza kufungwa jela kwa miaka saba.

Muswada huo ulipitishwa kwa wingi wa kura. Ni mbunge mmoja tu aliyepinga.

Mheshimiwa Fox Odoi alisema kuwa kuamua kutowafanya kuwa uhalifu watu wanaoonekana kuwa wapenzi wa jinsia moja ni kukiri kwamba wachache hawa wanaondoka Uganda na kwamba ni wajibu wa serikali kulinda haki zao.

Muswada huo umelaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu.

Sheria sawa na hiyo ilitupiliwa mbali na mahakama ya kikatiba ya nchi hiyo mwaka wa 2014.