Serikali ya wanamgambo wa Talibani imeendeleza ubabe wa jinsia ya kiume na kuzidi kuikandamiza ya kike nchini Afghanistan.
Agizo la hivi karibuni la kufungwa kwa saluni zote za urembo nchini humo limetajwa kuwa ukandamizaji mkubwa unaoendelea dhidi ya wanawake.
Kwa mujibu wa runinga ya CNN, Saluni za urembo nchini Afghanistan zimepewa muda wa mwezi mmoja kufungwa huku viongozi wa Taliban nchini humo wakipanua utawala wao dhalimu dhidi ya wanawake, ambao tayari kwa kiasi kikubwa wamezuiliwa majumbani mwao kwa kupigwa marufuku kazi nyingi na masomo.
Mohammad Sidik Akif Mahajar, msemaji wa Wizara ya Kueneza Wema na Kuzuia Mabaya, alithibitisha kwa CNN agizo hilo lilitolewa mnamo Juni 24, na saluni zote kufungwa hadi Julai 27.
Tangu kuchukua tena udhibiti wa nchi mnamo Agosti 2021, kufuatia kujiondoa kwa kwa Marekani na washirika wake, Taliban imerudisha nyuma miongo kadhaa ya maendeleo juu ya haki za binadamu.
Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa, Taliban imefanya "ukiukaji mkubwa wa utaratibu wa haki za wanawake," kwa kuzuia upatikanaji wao wa elimu na ajira na uwezo wao wa kutembea kwa uhuru katika jamii.
Kufungwa kwa saluni za urembo kunapunguza zaidi uhuru wa wanawake na kutoa pigo kali la kiuchumi kwa familia zinazowategemea kwa mapato.
Mmiliki wa saluni huko Kabul, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za usalama, aliiambia CNN kuwa bado hajapokea arifa ya maandishi ya agizo hilo lakini ripoti ambazo angelazimika kufunga zilimshtua.
"Sijui jinsi ya kuelezea hisia zangu. Mume wangu hana kazi na saluni hii ndiyo njia pekee ya kulisha familia yangu. Nina watoto wanne. Wanahitaji chakula, nguo na gharama za shule,” alisema.
"Sielewi kwa nini saluni zipigwe marufuku. Hakuna mwanamke anayeonyesha uso wake kwa kujipodoa nje. Tayari wamevaa hijabu hadharani. Hatua hii haitaondoa tu mapato ya familia nyingi, lakini itazidi kuwanyima wanawake haki na uhuru wao.”