Msiponipigia kura mtateseka – Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa

Licha ya hayo, rais alithibitisha kwamba hakuna mtu atakayemzuia yeye au chama chake kushinda uchaguzi huo

Muhtasari
  • Bw Mnangagwa pia aliwaambia wafuasi wake kwamba watateseka ikiwa wataupigia kura upinzani, ambao aliutaja kuwa umeshindwa.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa siku ya Jumatano amewaambia Wazimbabwe kwamba watapata shida ikiwa watashindwa kumchagua tena, katika wito wa wazi kuwataka kumpigia kura katika uchaguzi ujao.

Bw Mnangagwa pia aliwaambia wafuasi wake kwamba watateseka ikiwa wataupigia kura upinzani, ambao aliutaja kuwa umeshindwa.

Licha ya hayo, rais alithibitisha kwamba hakuna mtu atakayemzuia yeye au chama chake kushinda uchaguzi huo, huku kukiwa na shutuma za ukandamizaji wa kisiasa na vitisho dhidi ya wanasiasa wa upinzani na tuhuma za wizi wa kura uliopangwa.

"Sisi, Zanu-PF, hatutasimama na kuwaacha watu wetu wateseke mikononi mwa mabaraza haya yanayoongozwa na upinzani.

Lazima tuwafukuze tarehe 23 Agosti," aliwaambia zaidi ya wafuasi 150,000 waliohudhuria mkutano wake wa kampeni katika mji mkuu wa Harare.

Kwa mujibu wa rais, Zanu-PF, ambayo imetawala Zimbabwe tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 1980, ndicho chama pekee chenye uwezo wa kuongoza nchi hiyo.

Zimbabwe iko tayari kwa uchaguzi wa rais na bunge tarehe 23 Agosti.

Kinyang'anyiro cha urais kinahusisha wagombeaji 11, akiwemo rais aliyeko madarakani mwenye umri wa miaka 80 na Nelson Chamisa mwenye umri wa miaka 45, anayeongoza Chama cha Wananchi (CCC) na ambaye Wazimbabwe wengi wanamwona kuwa mpinzani wa kutisha zaidi kwa Bw Mnangagwa.

Bw Mnangagwa alichukua rasmi urais wa Zimbabwe mwaka 2018, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa madarakani dikteta Robert Mugabe mwaka wa 2017, na kumaliza utawala wake wa miaka 37 wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Wakati wa utawala wake, Wazimbabwe wameendelea kukabiliana na changamoto za kihistoria za mfumuko mkubwa wa bei na umaskini uliokithiri na ukosefu wa ajira.