Mapinduzi ya Gabon: Rais Ali Bongo aomba msaada akiwa katika kizuizi cha nyumbani

Akizungumza siku ya Jumatano kutoka kwa kile alichosema ni makazi yake, aliwataka wafuasi "kupaza sauti zao".

Muhtasari

•Ali Bongo ameomba msaada baada ya jeshi kumuondoa madarakani katika mapinduzi na kumuweka katika kizuizi cha nyumbani.

•Kupinduliwa kwa Bw.Bongo kutamaliza utawala wa familia yake uliodumu kwa miaka 55 madarakani nchini Gabon.

Image: BBC

Rais wa Gabon Ali Bongo ameomba msaada baada ya jeshi kumuondoa madarakani katika mapinduzi na kumuweka katika kizuizi cha nyumbani.

Akizungumza siku ya Jumatano kutoka kwa kile alichosema ni makazi yake, aliwataka wafuasi "kupaza sauti zao".

Hapo awali, maafisa wa jeshi walionekana kwenye TV na kusema wamechukua mamlaka.

Walisema walikuwa wamebatilisha matokeo ya uchaguzi wa Jumamosi ambapo Bw Bongo alitangazwa mshindi, lakini upinzani ulidai kuwa ulikuwa wa udanganyifu.

Maafisa hao pia walisema wamemkamata mmoja wa wanawe Bw.Bongo kwa kosa la uhaini.

Baadaye, walitangaza kwamba nafasi ya Bw.Bongo itachukuliwa na mkuu wa walinzi wa rais, Jenerali Brice Oligui Nguema, ambaye awali alibebwa kwa ushindi katika mitaa ya mji mkuu Libreville.

Walisema kuwa kuanzia Alhamisi, "watu wa Gabon watakuwa huru tena kufanya shughuli zao kati ya saa kumi na mbili asubuhi na saa kumi na mbili jioni", lakini vikwazo vya trafiki vitaendelea kuwepo kwa sasa.

Kupinduliwa kwa Bw.Bongo kutamaliza utawala wa familia yake uliodumu kwa miaka 55 madarakani nchini Gabon.

Nchi hiyo ni mojawapo ya wazalishaji wakuu wa mafuta barani Afrika, wakati karibu 90% yake imefunikwa na misitu. Ilijiunga na Jumuiya ya Madola mnamo Juni 2022, na kuwa mmoja wa wanachama wachache ambao hawakuwa koloni la Uingereza.

Katika ujumbe wake wa video, Bw Bongo alithibitisha kuwa alikuwa katika kizuizi cha nyumbani.

"Mwanangu yuko mahali fulani, mke wangu yuko sehemu nyingine ... Hakuna kinachoendelea. Sijui kinachoendelea," alisema kwa Kiingereza, kabla ya kuomba tena msaada.

Kampuni ya mawasiliano iliyokuwa ikifanya kazi kwa rais wakati wa uchaguzi imekuwa ikiwasiliana na BBC ili kuthibitisha ukweli wa picha hizo. Ilisema kuwa iliombwa na ofisi ya Bw.Bongo kusambaza video hiyo.

Katika taarifa yao kwa njia ya Televisheni, viongozi hao wa mapinduzi walisema wanafuta matokeo ya uchaguzi na kufuta "taasisi zote za jamhuri".

Mipaka ya nchi ilikuwa imefungwa "hadi ilani zaidi", waliongeza.

Hatua hiyo Ilikuja baada ya tume ya uchaguzi ya Gabon kusema kuwa Bw Bongo alipata ushindi chini ya theluthi mbili tu ya kura katika uchaguzi wa Jumamosi, ambao upinzani ulidai kuwa ulikuwa wa udanganyifu.

Mmoja wa wanajeshi hao alisema "wamekomesha utawala wa sasa" kwa sababu ya "utawala usiowajibika, usiotabirika na kusababisha kuzorota kwa mshikamano wa kijamii ambao unahatarisha nchi kutumbukia katika machafuko".

Image: BBC

Haya ni mapinduzi ya nane katika makoloni ya zamani ya Ufaransa barani Afrika katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Nchini Gabon hakuna shaka kwamba kwa kuwa wamekaa madarakani tangu 1967, wengi wametosheka na ukoo wa Bongo. Watu walikuwa wepesi kuingia barabarani, wakionekana kuwa na furaha ya kweli. Kufikia sasa, kuna ishara kidogo ya kurudi nyuma.

Serikali ya Ufaransa imelaani unyakuzi huo huku msemaji wake akitaka matokeo ya uchaguzi kuheshimiwa.

Hata hivyo, ushawishi wa Ufaransa barani Afrika umepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, na wito wa Ali Bongo kwa miaka mingi bado hauwezi kupungua.

Huenda wanajeshi wakaona mamlaka ya Ufaransa yakipungua na kuhisi kuwa na uwezo wa kuingilia kati kwa sababu hiyo, huku Paris ikiwa na uwezekano mdogo wa kumuunga mkono Bw Bongo.

Utumiaji wa Kiingereza wa Bw Bongo kwenye video yake, badala ya Kifaransa ambayo ni lugha rasmi ya Gabon, unaonesha kuwa alikuwa akihutubia Jumuiya ya Madola badala ya Ufaransa.

Urusi na China ni miongoni mwa nchi nyingine ambazo zimeelezea wasiwasi wao.

Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya amesema kutwaa mamlaka ya kijeshi kutaongeza ukosefu wa utulivu barani Afrika.

"Hili ni suala kubwa kwa Ulaya," Josep Borrell alisema.

Ufikiaji wa mtandao ulisitishwa kufuatia uchaguzi wa Jumamosi kwa sababu za kiusalama, lakini ukarejeshwa muda mfupi baada ya kuchukuliwa mamlaka. Amri ya kutotoka nje pia imewekwa.

Kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita nchini Gabon, kulikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mchakato wa kura ya Jumamosi.

Mgombea mkuu wa upinzani Albert Ondo Ossa alilalamika kuwa vituo vingi vya kupigia kura havikuwa na karatasi za kupigia kura zenye jina lake, huku muungano anaowakilisha ukisema majina ya baadhi ya waliojiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais bado yako kwenye karatasi.

Wanahabari wasio na mipaka, Reporters Without Borders wamesema vyombo vya habari vya kigeni vimepigwa marufuku kuingia nchini humo ili kuripoti kura.

Ushindi wote wa awali wa Bw.Bongo ulipingwa na wapinzani kuwa ulaghai.

Wakati huu, mabadiliko yenye utata yalifanywa kwa karatasi za kupigia kura wiki chache kabla ya siku ya uchaguzi.

Bw.Bongo aliingia mamlakani wakati baba yake Omar alipofariki mwaka 2009.

Mnamo mwaka wa 2018, alipatwa na kiharusi ambacho kilimuweka nje ya siasa kwa karibu mwaka mmoja na kusababisha wito wa kujiuzulu.

Mwaka uliofuata, jaribio la mapinduzi lililofeli lilishuhudia askari waasi wakipelekwa gerezani.