Elon Musk: Watumiaji wa X huenda wakaanza kutoa malipo ili kutumia jukwaa hilo,

Haijulikani ikiwa haya yalikuwa maoni tu ya pembeni, au ishara ya mipango thabiti ambayo bado haijatangazwa.

Muhtasari

• Ingawa kuna faida ya kifedha kwa kampuni hiyo kutoza watumiaji, Bw Musk alisisitiza kuwa kupata watu wa kulipia huduma hiyo kunalenga kukabiliana na roboti.

Elon Musk
Image: GETTY IMAGES

Elon Musk amependekeza kuwa watumiaji wote wa X, ambayo zamani iliitwa Twitter, wanaweza kulipa ili kufikia huduma za mtandao huo

Katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, bilionea huyo alisema mfumo wa malipo ndiyo njia pekee ya kukabiliana na utumizi wa akaunti zinazoendeshwa na roboti.

"Tunaelekea kuwa na malipo madogo ya kila mwezi kwa matumizi ya mfumo," bosi wa Tesla na SpaceX alisema.

BBC ilitaka maeleo Zaidi kutoka kwa X lakini bado haijapokea taarifa kutoka kwa kampuni hiyo.

Haijulikani ikiwa haya yalikuwa maoni tu ya pembeni, au ishara ya mipango thabiti ambayo bado haijatangazwa.

Bw Musk amekuwa akisema kwa muda mrefu kuwa suluhisho lake la kuondoa roboti na akaunti ghushi kwenye jukwaa la mitandao ya kijamii ni kutoza ada kwa watumaiji wake.

Tangu achukue umiliki wa Twitter mwaka jana ametafuta kuhamasisha watumiaji kulipia huduma iliyoboreshwa, ambayo sasa inaitwa X Premium.

Hili limefanywa kwa kuwapa watumiaji wanaolipia vipengele zaidi, kama vile machapisho marefu na kuongezeka kwa mwonekano kwenye jukwaa.

Walakini, watumiaji bado wanaweza kutumia X bila malipo.

Ingawa kuna faida ya kifedha kwa kampuni hiyo kutoza watumiaji, Bw Musk alisisitiza kuwa kupata watu wa kulipia huduma hiyo kunalenga kukabiliana na roboti.