Wanafunzi 400 waliokuwa wanasomea kozi ya uganga wa jadi wahitimu Tanzania

Wahitimu hao walipitia kozi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja katika chuo cha Modesta na baada ya kuhitimu, walipewa nguvu na uwezo wa kutoa tiba asili kwa wanaougua magonjwa mbalimbali.

Muhtasari

• Mbunge wa eneo hilo aliyekuwa mmoja wa waliohudhuria kuhafili kwao alisema kuwa watajaribu kadri ya uwezo wao kupeleka somo la kitamaduni shuleni katika mtaala mpya.

Mahafali wa uganga
Mahafali wa uganga
Image: Screengrab

Taifa la Tanzania limeingia katika vitabu vya historia kwa kutoa kundi la kwanza kabisa la wanafunzi ambao walikuwa wanasomea kozi ya uganga wa kienyeji.

Kwa mujibu wa Ayo TV, chuo cha uganga wa jadi cha Modesta kilichopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kimekuwa cha kwanza kabisa kutoa wahitimu wasiopungua 400 ambao walikuwa wanaandaliwa kwa mafunzo kabambe ya uganga wa kiasili.

Mahafali hayo yalihudhuriwa na umati wa watu Zaidi ya elfu moja kushuhudia kufuzu kwa wanafunzi hao ambao walipitia mafunzo ya uganga kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mbunge wa jimbo la Kahama, Jumanne Kishimba alitoa wito kwa serikali kukumbatia mafunzo hayo ya asili akisema kuwa ni sehemu ya tamaduni na wala hakuna mila, destruri na tamaduni zilizo potovu.

“Sasa hivi kwenye mtaala mpya wa elimu, tunapeleka suala la utamaduni shuleni na mimi ndiye nilikuwa nalipigania sana kwamba jamani tunahangaika. Mjini tunasema sijui tunaugua msongo wa mawazo, matatizo ya akili, sasa mbona kijijini hawaugui huo msongo wa mawazo? Kwa nini tusiende kwao tukawauliza kama nyinyi hamuugui ina maana hizi dawa mnazo. Tunajaribu kwa njia zote kuendeleza mila sahihi,” mbunge huyo alisema.

Taifa la Tanzania kwa muda mrefu limekuwa likijulikana kwa mila ya uganga wa kiasili ambao wengi wanaumini na vile vile kuuambatanisha na matukio ya ushirikina na uchawi.