Takriban watu 21 wafariki baada ya basi kuanguka kutoka kwenye daraja

Basi hilo lilivunja kizuizi na kutumbukia karibu na njia za reli katika wilaya ya Mestre, ambayo imeunganishwa na Venice kwa daraja.

Muhtasari

•Miongoni mwa waliofariki ni raia watano wa Ukraine, Mjerumani mmoja na dereva wa Italia, gavana wa jiji Michele Di Bari alisema.

•Takriban watu 18 wamejeruhiwa, watano kati yao vibaya sana.

Image: BBC

Takriban watu 21 wakiwemo watoto wawili wamefariki baada ya basi kuanguka kwenye barabara ya juu karibu na mji wa Venice nchini Italia na kuwaka moto, maafisa wamesema.

Basi hilo lilivunja kizuizi na kutumbukia karibu na njia za reli katika wilaya ya Mestre, ambayo imeunganishwa na Venice kwa daraja.

Miongoni mwa waliofariki ni raia watano wa Ukraine, Mjerumani mmoja na dereva wa Italia, gavana wa jiji Michele Di Bari alisema.

Meya wa Venice Luigi Brugnaro alisema "janga kubwa" limetokea.

"Hakuna maneno yanayoweza kueleza tukio hilo," alisema kwenye mtandao wa kijamii.

Basi hilo linafikiriwa kukodishwa kuchukua watalii kati ya Venice na eneo la kambi katika wilaya ya karibu ya Marghera.

Kisa hicho kilitokea mwendo wa saa 19:45 (17:45 GMT) huku basi hilo likiripotiwa kuwarudisha watalii kwenye kambi hiyo.

Baadhi ya ripoti zinasema basi hilo lilikuwa linatumia gesi ya methane na kuangukia kwenye njia za umeme na kuwaka moto.

Waziri wa Mambo ya Ndani Matteo Piantedosi alionya kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka.

Chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika na waokoaji wanaendelea na kazi nayo katika eneo la tukio.

Takriban watu 18 wamejeruhiwa, watano kati yao vibaya sana.

Kituo cha mapokezi chenye watalaam wa kisaikolojia na magonjwa ya akili kimeanzishwa katika hospitali iliyo karibu ili kutoa msaada kwa familia za waathiriwa.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni alisema anafuatilia matukio na akatoa rambirambi zake.

"Mawazo yetu ni kwa waathiriwa na familia zao na marafiki," alisema.

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema anasimama na viongozi wa Italia "wakati huu wa maumivu makali".

Mnamo mwaka wa 2013, watu 38 waliuawa baada ya dereva kushindwa kudhibiti njia karibu na mji wa Monteforte Irpino kusini mwa Italia, na kugonga magari mengine kadhaa kabla ya kuanguka kwenye korongo.