Wabunge wa Zimbabwe wapoteza viti kwa sababu ya barua bandia

Alipopokea barua hiyo ya ulaghai, spika wa bunge la Zimbabwe alitangaza kuwa viti 15 viko wazi.

Muhtasari

• Barua ya Jumatatu ilitiwa saini na "Sengezo Tshabangu", ambaye alidai kuwa katibu mkuu wa Citizens Coalition for Change (CCC).

Image: AFP

Wabunge 15 wa upinzani nchini Zimbabwe wamewasilisha rufaa mahakamani wakisema walidanganywa ili kupoteza viti vyao vya ubunge.

Hii imekuja baada ya mtu mmoja aliyedai kuwa Katibu wa chama hicho kwa uongo kusema kuwa wabunge hao si wanachama tena.

Alipopokea barua hiyo ya ulaghai, spika wa bunge la Zimbabwe alitangaza kuwa viti 15 viko wazi.

Matokeo ya uchaguzi mdogo yanaweza kukabidhi chama tawala cha Zanu-PF idadi kubwa inayohitaji kufanya marekebisho ya katiba.

Barua ya Jumatatu ilitiwa saini na "Sengezo Tshabangu", ambaye alidai kuwa katibu mkuu wa Citizens Coalition for Change (CCC), chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe.

Ilikuwa imejaa makosa ya kisarufi.

Kiongozi wa CCC Nelson Chamisa alimtaka spika Jacob Mudenda kupuuza barua hiyo akisema chama hicho hakina katibu mkuu na hakijamfukuza wala kumrudisha mbunge yeyote.