Waziri ataka bunge kupitisha mswada watu maskini kucharazwa viboko ili kutafuta utajiri

Waziri huyo alisema serikali imeweka mipango kabambe ya kuhakikisha wananchi wote wanaodnokana na tatizo la umaskini lakini bado kuna wengine wanariya na kusuasua na wanastahili kusukumwa.

Muhtasari

• Hii si mara ya kwanza kwa afisa mkuu wa serikali nchini humo kutoa matamshi ya hovyo kama hayo.

• Itakumbukwa mwezi Mei mwaka 2022 Waziri wa Masuala ya Ndani Kahinda Otafire alisema watu maskini hawataenda mbinguni.

Afisa wa serikali akiwachapa wafanyibiashara.
Afisa wa serikali akiwachapa wafanyibiashara.
Image: BBC NEWS

Waziri wa fedha nchini Uganda, Haruna Kasolo ameripotiwa kulitaka bunge kupitisha mswada wa kuruhusu watu maskini kuwekwa katika mpango wa kucharazwa viboko na mijeledi kila wakati ili kujibidiisha katika kutafuta kazi na kuwa matajiri.

Kwa mujibu wa ripoti ya Eye Radio ya nchini humo, waziri humo alisema kwamba uongozi wa serikali ya Museveni umeweka mipango kabambe ya kuhakikisha kwamba Waganda wanatokana na umaskini na hiyo ni njia moja ya kuhakikisha azma hilo linatimia.

“Rais Museveni na serikali ya NRM tumeweka mipango kabambe ya kutokomeza umaskini tukiwa na lengo la kuhakikisha kila Mganda anakuwa tajiri, lakini kuna wengine ambao wanasuasua na kusalia kuwa maskini,” sehemu ya hotuba ya waziri huyo ilinukuliwa.

“Huku mbeleni, huenda serikali ikalazimika kupitisha mswada ambapo watu wote maskini watakuwa wanatiwa viboko ili kujifunza jinsi ya kufanya kazi na pia kuwa matajiri kwa sababu tumegundua kwamba baadhi ya Waganda wanastahili kusukumwa katika mkondo wa kupata utajiri,” taarifa hiyo iliongeza.

Waziri huyo alikuwa anahutubia mkutano wa muungano wa wafanyibiashara wadogo wa Saccos ambapo dhima ilikuwa kuwapa watu hamasisho la jinsi ya kuwekeza mali zao.

Hii si mara ya kwanza kwa afisa mkuu wa serikali nchini humo kutoa matamshi ya hovyo kama hayo.

Itakumbukwa mwezi Mei mwaka 2022 Waziri wa Masuala ya Ndani Kahinda Otafire alisema watu maskini hawataenda mbinguni.

Waziri huyo alisema wanaoendelea kuwaombea kwa Mungu ili waondokane na umaskini wanamsumbua Mungu kwa sababu walipewa mikono ya kufanya kazi na pia kuwa matajiri.

Aliyasema hayo katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Biashara ya St Klaus Comprehensive katika kijiji cha Bufunjo, halmashauri ya mji wa Kifuko wilayani Kyenjojo, Magharibi mwa Uganda.

Alikuwa akiwaeleza wanafunzi kuwa kufanya kazi kwa bidii ndio dawa ya umaskini ambapo alitoa matamshi hayo yenye virusi.

“Maskini hawataenda mbinguni kwa sababu wanamtukana Mungu kwa maombolezo na shutuma kila siku,” Waziri alisema.