Familia za mateka 13 wa Israel walioachiwa huru na Hamas zimezelezea jinsi zilivyofarijika baada ya jamaa zao kurejea nyumbani.
Kundi hilo la mateka, ambalo linajumuisha watoto wadogo na wanawake wazee, sasa wamerejea nchini Israel baada ya kusafirishwa na Shirika la Msalaba Mwekundu kutoka Gaza hadi Misri.
Muda mfupi baadaye, wafungwa 39 wa Kipalestina waliachiliwa kupitia kituo cha ukaguzi cha Beitunia katika Ukingo wa Magharibi.
Raia kumi wa Thailand na Mfilipino mmoja pia waliachiliwa huru na Hamas, katika mkataba tofauti na ule uliopatanishwa na Qatar.
Chini ya makubaliano ya Qatar, jumla ya mateka 50 wa Israel na wafungwa 150 wa Kipalestina wanakusudiwa kuachiwa huru katika muda wa siku nne wakati wa usitishaji mapigano kwa muda.
Mateka walioachiwa na Hamas siku ya Ijumaa walipelekwa katika hospitali ya Misri kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kabla ya kurudishwa Israel.
Waisraeli hao ni pamoja na watoto wanne - walio na umri wa miaka miwili, minne, sita na tisa - pamoja na mwanamke mwenye umri wa miaka 85.
"Sasa tumekamilisha awamu ya kwanza ya kuwarejesha mateka wetu. Watoto, mama zao na wanawake wengine. Kila mmoja wao ni ulimwengu mzima," Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema.
"Lakini ninasisitiza kwenu - familia, na kwenu - raia wa Israel: Tumejitolea kuwarudisha mateka wetu wote."
Mke wa Yoni Asher, Doron Katz Asher, 34, na binti zao wawili Raz, wanne, na Aviv, wawili, wameachiliwa.
"Nimeazimia kufufua familia yangu kutoka kwa kiwewe na msiba mbaya tuliopitia," Bw Asher aliambia BBC.
"Sifanyi sherehe, sitasherehekea hadi wote waliotekwa warudi," alisema.
“Familia za waliotekwa si mabango, si kauli mbiu, ni watu halisi, na familia za waliotekwa kuanzia leo ni familia yangu mpya, na nitahakikisha na kufanya kila niwezalo kuhakikisha watu wote waliotekwa wanarudi nyumbani. "
Margalit Moses, 78, pia alikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa na Hamas. Manusura wa saratani, alitekwa nyara kutoka Kibbutz Nir Oz na Hamas tarehe 7 Oktoba.
Daniele Aloni na bintiye Emilia mwenye umri wa miaka sita pia wameachiliwa kama sehemu ya mkataba huo. Walitekwa nyara tarehe 7 Oktoba wakati wa ziara ya kukaa na familia huko Kibbutz Nir Oz.
Wakati wa mashambulizi, ujumbe wa mwisho Daniele aliotuma kwa familia yake ulisema kwamba "kulikuwa na magaidi katika nyumba yao" na aliohofia kwamba hawatapona.
Itay Ravi, ambaye binamu yake Avraham mwenye umri wa miaka 78 bado anazuiliwa, anasema "hii ni hatua moja kuelekea kuwa na furaha" baada ya jamaa zake watatu kuachiwa huru.
Shangazi yake, Ruthi Munder, 78, binamu yake Keren Munder, 54, na mwanawe, Ohad Munder-Zichri, tisa, walitekwa nyara kutoka Nir Oz.
"Wanaelekea katika hospitali za Israel, kwa familia, na hii inasisimua sana. Hata hivyo, hatuwezi kuwa na furaha kabisa," aliiambia BBC Newsnight.
Ohad alitimiza miaka tisa alipokuwa akizuiliwa huko Gaza.
"Sherehe pekee ambayo tutafanya hivi karibuni ni [ya] siku ya kuzaliwa ya tisa ya Ohad," Bw Ravi alisema.
"Sasa tutakuwa na sherehe kubwa kwa ajili yake, pamoja na marafiki na familia, baada ya tukio hili. Tutaona jinsi atakavyorudi ... sijui jinsi mtoto wa miaka tisa anakuja. nyuma baada ya siku 50 mikononi mwa shirika la kigaidi. Natumai atafanya vyema."
Pia kulikuwa na ahueni kubwa miongoni mwa familia za raia wa Thailand na Wafilipino walioachiwa na Hamas.
Kittiya Thuengsaeng, mpenzi wa mateka wa Thailand mwenye umri wa miaka 28, Wichai Kalapat, alielezea hali ngumu aliyopitia tangu alipotoweka.
Aliambiwa na maafisa wa Thailand kwamba mpenzi wake wa miaka mitatu alikufa katika mashambulizi ya Oktoba 7. Lakini mamlaka ya Thailand ilipotangaza majina yote ya marehemu, jina la Wichai halikuwepo hapo.
Siku tano zilizopita, aliambiwa alikuwa kwenye orodha ya mateka wa Thailand.
Gelienor (Jimmy) Pacheco, 33, kutoka Ufilipino, alichukuliwa kutoka Kibbutz Nir Oz mnamo Oktoba 7. Jimmy alikuwa mlezi wa mkazi wa kibbutz Amitai Ben Zvi ambaye aliuawa katika uvamizi wa Hamas.
Maelezo ya Wichai na Jimmy yalithibitishwa Jumamosi asubuhi.
Jumla ya wafungwa 39 wa Kipalestina wameachiliwa kutoka jela za Israel kama sehemu ya makubaliano hayo.
Wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali, kuanzia kurusha mawe hadi kujaribu kuua. Baadhi walikuwa wamehukumiwa kwa uhalifu huku wengine wakisubiri kesi zao kusikilizwa.
Kundi hilo la wanawake 24 na wavulana 15 liliachiliwa katika kizuizi cha Beituniya katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na kulakiwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wakiimba.
Mfungwa mmoja wa Kipalestina aliyeachiliwa huru ni Marah Bakeer. Alikamatwa mwaka wa 2015, alipokuwa na umri wa miaka 16, na alihukumiwa kifungo cha miaka minane na nusu jela kwa shambulio la kisu dhidi ya afisa wa polisi wa mpaka.
Bakeer aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri: "Mkataba huu unakuja kufuatia kifo cha watu wengi na hii inatufanya tukose furaha na kukosa raha."
Alisema aliwekwa katika kifungo cha upweke na "hakujua kinachoendelea nje, wala hajui kuhusu hali ya Gaza".
"Habari za mpango huo zilishangaza," alisema.
Wafungwa hao walichaguliwa kutoka katika orodha ya wanawake na watoto 300 iliyoandaliwa na Israel.
Chini ya robo ya wale walio kwenye orodha wamehukumiwa - wengi wao wanazuiliwa rumande wakisubiri kesi zao kusikilizwa. Wengi wa walioorodheshwa ni wavulana waliobalehe- 40% yao chini ya umri wa miaka 18. Pia kuna msichana mmoja na wanawake 32.
Hamas iliwachukua mateka zaidi ya 200 wakati wa shambulio la kuvuka mpaka kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba ambapo watu 1,200 waliuawa.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa idadi ya Wapalestina wanaoshikiliwa bila kufunguliwa mashtaka katika jela za Israel imeongezeka tangu mashambulizi ya Oktoba 7.
Jumla ya malori 60 ya misaada yameingia Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano - Israel inasema malori manane yanaleta mafuta, sehemu ya lita 130,000 zitakazowasilishwa kila siku ya mapatano.
Ingawa makubaliano ya siku nne ya kusitisha mapigano yanapendekeza maeneo yote yafikiwe na mashirika ya misaada, Israel imewaambia Wapalestina waliokimbia makazi yao kusini mwa nchi wasijaribu kurejea nyumbani, ikisema kaskazini ni eneo la vita - ingawa maelfu ya raia wanaaminika kusali huko.