Wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa kutoka jela za Israel wameiambia BBC kwamba walinzi waliwanyanyasa na kuwapa adhabu ya pamoja wiki chache baada ya mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba.
Wafungwa hao - ambao waliachiliwa wiki iliyopita kama sehemu ya makubaliano ya mateka ambayo sasa yamekamilika - wameelezea kuchapwa kwa fimbo, kuwekewa mbwa waliofungwa midomo, na nguo zao, chakula na blanketi kuchukuliwa.
Mfungwa mmoja wa kike amesema alitishiwa kubakwa, na kwamba walinzi waliwarushia mabomu ya kutoa machozi mara mbili ndani ya seli.
BBC ilizungumza na watu sita kwa jumla, ambao wote walisema walipigwa kabla ya kuondoka jela.
Jumuiya ya Wafungwa wa Kipalestina inasema baadhi ya walinzi wanadaiwa kuwakojolea wafungwa waliofungwa pingu na kwamba wafungwa sita walifariki wakiwa jela.
Kujibu madai hayo, Jeshi la Magereza la Israel liliambia BBC wafungwa wote walizuiliwa kwa mujibu wa sheria na walikuwa na haki zao zote za kimsingi zinazohitajika kisheria.
"Hatujui madai uliyoelezea," ilisema katika taarifa. "Hata hivyo, wafungwa na waliozuiliwa wana haki ya kuwasilisha malalamiko ambayo yatachunguzwa kikamilifu na mamlaka rasmi."
Israel haikuzungumzia swali letu kuhusu vifo wakiwa kizuizini moja kwa moja, lakini ilisema kuwa wafungwa wanne walifariki kwa tarehe nne tofauti katika wiki zilizopita, na kwamba huduma ya magereza haikuwa na ufahamu wa sababu za kifo.