Aliyekuwa Rais wa Mauritania Aziz afungwa miaka mitano jela kwa ufisadi

Mohamed Ould Abdel Aziz anadaiwa kujilimbikizia mali nyingi wakati wa utawala wake wa miaka 10.

Muhtasari

•Mahakama nchini Mauritania imemfunga rais wa zamani Mohamed Ould Abdel Aziz kifungo cha miaka mitano kwa kosa la rushwa.

Image: BBC

Mohamed Ould Abdel Aziz, aliyeonekana hapa mwaka 2018, anadaiwa kujilimbikizia mali nyingi wakati wa utawala wake wa miaka 10.

Mahakama nchini Mauritania imemfunga rais wa zamani Mohamed Ould Abdel Aziz kifungo cha miaka mitano kwa kosa la rushwa.

Ilimpata Aziz na hatia ya utakatishaji fedha na kutumia nafasi yake vibaya ili kujitajirisha kinyume cha sheria, lakini ilimwachilia huru kwa mashtaka mengine.

Mahakama pia iliamuru kutaifishwa kwa mali yake aliyoipata kinyume cha sheria.

Aziz, mwenye umri wa miaka 66, alichaguliwa kuwa rais mwaka wa 2009 baada ya kumg’oa madarakani Rais Sidi Ould Cheikh Abdallahi katika mapinduzi, na akaendelea kuiongoza Mauritania hadi 2019.

Alikuwa ameshtakiwa katika mji mkuu, Nouakchott, tangu Januari, pamoja na watu wengine 10 mashuhuri, wakiwemo mawaziri wakuu wawili wa zamani na mawaziri wa zamani waliohudumu katika utawala wake.

Walikuwa wameshtakiwa kwa makosa kadhaa, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka, utakatishaji fedha, kujitajirisha haramu na kufanya biashara ya ushawishi.

Mahakama hiyo ambayo ni mtaalamu wa masuala ya rushwa na uhalifu wa kiuchumi, pia iliwahukumu baadhi ya washtakiwa wenza siku ya Jumatatu, japo kwa adhabu nyepesi kuliko Aziz, huku mawaziri wakuu wa zamani na mawaziri wawili wa zamani wakiachiliwa huru.

Aziz alidumisha kutokuwa na hatia katika kipindi chote cha kesi hiyo na alielezea mashtaka yake kama yalichochewa kisiasa.

Inasemekana kuwa alitofautiana na mrithi wake na Rais wa sasa Mohamed Ould Ghazouani, ambaye wakati mmoja alikuwa mshirika wake wa karibu wa kisiasa, shirika la habari la AFP linaripoti.