Bei ya mafuta yaendelea kushuka Tanzania

Kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo kunadaiwa kuchangiwa na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la duniani.

Muhtasari

•Watanzania wanaendelea kupata ahueni na kupunguza kiwango cha fedha wanachotumia katika kununua mafuta baada ya bei kuendelea kushuka nchini.

Image: BBC

Watumiaji wa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini Tanzania wanaendelea kupata ahueni na kupunguza kiwango cha fedha wanachotumia katika kununua bidhaa hiyo baada ya bei kuendelea kushuka nchini.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi nchini Tanzania, Kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo mwaka huu kunadaiwa kuchangiwa na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la duniani kwa asilimia 10 kwa petroli , asilimia 11 kwa dizeli na asilimia 5.8 kwa mafuta ya taa.

Pia kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo kumechangiwa na kushuka kwa gharama ya uagizaji wa mafuta katika bandari ya Dar es salaam kwa wastani wa asilimia 9.69 kwa dizeli na asilimia 1.82 kwa mafuta ya taa.

Taarifa ya bei hiyo mpya inayoanza kutumika leo tarehe saba mwezi Februari iliotolewa na mamlaka ya udhibiti wahuduma za nishati na maji Ewura inaelezea gharama za uagizaji wa mafuta ya petroli na dizeli katika bandari ya Tanzana na Mtwara , nazo zimepungua kwa asilimia 0.69 na asilimia 11.93 mtawalia.

Kufuatia hatua hiyo sasa wakaazi wa Dar es Salaam watanunua lita moja ya mafuta ya petroli kwa bei isiozidi sh. 3,051 kutoka sh. 3,084 iliokuwepo awali. Bei ya Mafuta ya taa nayo imeshuka hadi 284 kutoka sh.3,501 ilisema Mwananchi.